Mchengerwa anusa ubadhirifu Lindi, atoa maagizo

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa pamoja na viongozi wengine wakati akivuta kitambaa kuweka jiwe la Msingi Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Lindi katika Kijiji cha Kilangala Mkoani humo tarehe 19 Septemba, 2023.

What you need to know:

  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi kupeleka wataalamu mkoani Lindi kuchunguza ubadhirifu wa fedha.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ameibua sakata la ubadhirifu uliofanywa na watendaji wa manispaa ya Lindi akieleza wametumi madaraka yao vibaya kwenda kukopa fedha bila kufuata utaratibu.

Mchengerwa ameyasema hayo leo Jumanne, Septemba 19, 2023 wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan iliyomalizika mkoani Lindi. Hata hivyo, waziri huyo hakuweka wazi kiasi cha fedha kilichokopwa na matumizi yake.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais, Mchengerwa amesema,“hapa katika manispaa ya Lindi kuna ubadhirifu wa fedha, kuna matumizi mabaya ya madaraka. Manispaa wamekwenda kukopa fedha bila kufuata taratibu.”

Amesema kufuatia hilo, amemuelekeza Katibu Mkuu wa Tamisemi kuhakikisha kufikia Jumatatu awe amepeleka watalaam kwenda kufanya uchunguzi wa fedha hizo ambazo zimekopwa bila kufuata utaratibu.

“Niwaombe Watanzania na wasaidizi wangu kote nchi nzima kuhakikisha kwamba huu ni wakati wa kufanya kazi kuwatumikia wananchi, kila mmoja wote ajikite katika msingi wa uadilifu afanye kazi kwa ajili ya Watanzania,” amesema Mchengerwa.


Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, Rais Samia anashangaa kuona Lindi inaendelea kuwa nyuma licha ya fursa zilizopo kwenye mkoa huo.

“Lindi ni miongoni mwa mikoa yenye fursa nyingi, kinachoonekana fursa hizi hazijatumiwa vyema. Binafsi nashindwa kuelewa kwanini Lindi awepo kijana ambaye hana ajira, kwa fursa zilizopo ilitakiwa kila kijana awe na ajira au ajiajiri, jipangeni mjiweke sawa,” amesema

“Hapa wabunge wenu wameomba vitu vingi bila kujua fedha zinatoka wapi, sasa niwakumbushe wana Lindi fanyeni kazi kwa bidii ili zipatikane fedha ambazo tutazitumia kwenye maendeleo. Nimepita mchana naona wengine wapo kwenye vijiwe na ni muda wa kazi niwaombe wana Lindi acheni uvivu tuamke tufanye kazi,” amesema