Mchengerwa ataka tembo wasakwe kwa helkopita

Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Kalemawe wilayani Same
Muktasari:
Waziri wa Maliasili na Utalii, nchini Tanzania, Mohamed Mchengerwa ametoa siku tatu kwa Shirika la hifadhi za Taifa (Tanapa) kuhakikisha wanapeleka helkopta wilayani Same na kufanya operesheni ya kuwaondoa tembo ambao wamevamia mashamba na makazi ya watu na kuwarudisha ndani ya hifadhi.
Same. Waziri wa Maliasili na Utalii, nchini Tanzania, Mohamed Mchengerwa ametoa siku tatu kwa Shirika la hifadhi za Taifa (Tanapa) kuhakikisha wanapeleka helkopta wilayani Same na kufanya operesheni ya kuwaondoa tembo ambao wamevamia mashamba na makazi ya watu na kuwarudisha ndani ya hifadhi.
Migongano baina ya wanyamapori hususani Tembo na binadamu imekuwa ni tatizo kubwa katika maeneo yanayozunguka hifadhi za wanyamapori ambapo kwa Mkoa wa Kilimanjaro kilio kikubwa kiko Wilaya ya Same na Mwanga.
Mbali na Helkopta, pia waziri ameagiza wananchi wanaodai fidia katika Wilaya ya Same kulipwa Wiki ijayo, ambapo kwa Wilaya hiyo, wananchi 1,538 wanadai fidia kutokana na uharibifu wa mazao na vifo vilivyotokana na Tembo.
Mchengerwa ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za kumnadi mgombea udiwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kata ya Kalemawe Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Jofrey Mtwa Jofrey.
Ameema serikali imejipanga vizuri kuhakikisha Tembo wote wanaondoka katika maeneo ya wananchi na kurudishwa ndani ya hifadhi haraka iwezekanavyo ili wananchi waishi kwa amani, hivyo ni jukumu la viongozi waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi kuhakikisha wanafanya kazi kwa kasi inayohitajika.
"Nimeambiwa wananchi hapa mnasumbuliwa sana na tembo, sasa nawaagiza Tanapa ndani ya siku hizi mbili, tatu, mhakikishe mnaleta helkopta hapa na kuondoa wanyama hao na kuwarudisha ndani ya hifadhi, na operesheni hiyo ianze mara moja,” amesema na kuongeza;
"Lakini pia nimeambiwa hapa kuna wananchi wanadai fidia, kuna ambao mazao yao yameliwa na kuna ambao wamepoteza maisha, Serikali yetu ni sikivu, fedha ya fidia ipo na niwahakikishie wananchi wa Same tutajitahidi wiki ijayo wote wanaodai fidia wawe wamelipwa"
Wakizungumza baadhi ya wananchi wa Kalemawe wamesema uvamizi wa tembo katika mashamba na
Naye Ester Moses amesema tembo wamekuwa wengi katika maeneo ya wananchi na hivyo kuhatarisha maisha yao hasa kwa wanafunzi pindi wanapokwenda shule.
Kata ya Kalemawe ni miongoni mwa kata 14 za Tanzania Bara, zilizotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufanya uchaguzi mdogo wa Madiwani, ambao unatarajiwa kufanyika Julai 13, mwaka huu.