Mchungaji aeleza alivyojiandaa ndoa ya marehemu Rehema
Muktasari:
- Rehema ambaye alikuwa ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Sua, yeye na pamoja na mama yake, walifariki Novemba 28, 2023 yeye, mama yake pamoja na mfanyakazi wa ndani Irene Shija (15), baada ya gari alilokuwa akiendesha bibi harusi huyo, kugongana na lori.
Moshi. Mchungaji wa Usharika Oldonyosambu, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Daniel Ole Kambaine ameeleza namna alivyokuwa amejipanga kufungisha ndoa ya marehemu Rehema Chao (39) ambayo ingefanyika leo Desemba 2, 2023.
Mchungaji Kambaine ameyasema hayo wakati mamia ya waombolezaji kutoka maeneo mbalimbali nchini, wakishiriki ibada ya maziko ya bibi harusi huyo mtarajiwa na mama yake mzazi, Agness Chao (75) ambao walifariki kwa ajali ya gari wakitokea mkoani Morogoro, kwenye sherehe za send-off ya Rehema (marehemu).
Rehema ambaye alikuwa ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Sua, yeye na pamoja na mama yake, walifariki Novemba 28,2023 yeye, mama yake pamoja na mfanyakazi wa ndani Irene Shija (15), baada ya gari alilokuwa akiendesha bibi harusi huyo, kugongana na lori.
Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Kichwa cha Ng'ombe, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, wakati dereva (Rehema) akijaribu kukwepa shimo.
"Niliandikisha ndoa ya Aman Mollel na Rehema Chao (Marehemu) na leo ilikuwa niifunge harusi yao Usharika wa Oldonyosambu Arusha, lakini Mungu hakuamua tufunge harusi, ameamua tuje kwenye harusi nyingine," amesema Mchungaji Kambaine.
Kauli ya Mchungaji huyo wa Usharika wa Oldonyosambu mkoani Arusha, ameitoa katika usharika wa Nganyeni wa kanisa hilo, wakati wa ibada ya maziko ya Rehema na mama yake, kauli ambayo imeibua vilio kutoka kwa mamia ya waombolezaji waliofika kanisani hapo.
Mchungaji amesema Aman alimpenda Rehema (marehemu) na alitegemea leo Desemba 2, awe mke wake lakini Mungu amempenda zaidi.
"Mungu hakuamua tufunge harusi, ameamua tuje kwenye harusi nyingine, Aman alimpenda Rehema na alitegemea leo awe Mke wake, lakini haikuwa hivyo Mungu amempenda zaidi, tumuachie Mungu awe faraja," amesema Mchungaji.
Rehema alichumbiwa na kuvishwa pete na Mchumba wake Aman Mollel Septemba 2, 2023 na Novemba 24, mwaka huu, alifanyiwa sherehe ya kugawa (Send-off) mkoani Morogoro.