Harusi iliyogeuka kuwa msiba
Amani Mollel (wa kwanza kulia), akiwa amebeba msalaba wa Rehema Chao, ambaye alikuwa anatarajia kufunga ndoa leo Jumamosi Desemba 2, 2023. Picha na Janeth Joseph.
Muktasari:
- Leo Desemba 2, 2023 ndio ilikuwa iwe harusi kati ya Rehema Chao na Amani Mollel na ilitarajiwa kufungwa katika usharika wa Oldonyosambo mkoani Arusha, lakini kufuatia ajali iliyoondoa uhai wa bibi harusi na nduguze, leo furaha imegeuka kilio.
Moshi. Imekuwa ni wakati mgumu kwa Amani Mollel aliyekuwa bwana harusi mtarajiwa wa Rehema Chao (37) aliyefariki ajalini wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, akitokea kwenye ‘Send-off’ yake iliyofanyika mkoani Morogoro Novemba 24, 2023.
Rehema aliyekuwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Sua, mkoani Morogoro, ambaye alikuwa akiendesha gari lilipata ajali Novemba 28, mwaka huu na kuchukua uhai wake, mama yake mzazi, Agness Chao (75) pamoja na msichana wa kazi Irene Shija, huku mdogo wake na mwanaye wakijeruhiwa.
Hata hivyo, leo wakati mwili ukitolewa nyumbani kwao kijiji cha Nganyeni kata ya Mwika Kaskazini, Molel alishindwa kujizuia kulia hali ambayo iliibua vilio kwa mamia ya waombolezaji waliofika kwa ajili ya kushiriki katika ibada ya maziko ya Rehema na mama yake, ambayo yanafanyika leo nyumbani kwao.
Mwili wa Rehema umeagwa kwa kuangaliwa picha baada ya familia kueleza kuwa mwili wake umeharibika kutokana na ajali hiyo, huku mwili wa mama yake ukiangaliwa.
Ajali hiyo ilitokea eneo la Kichwa cha Ng'ombe wilayani Mwanga, baada ya gari aliyokuwa akiendesha Rehema (marehemu) aina ya Raumu akiwa na mama yake na ndugu wengine kugongana na lori wakati akijaribu kukwepa shimo.
Ibada ya maziko inafanyika katika usharika wa Nganyeni wilaya ya Moshi na baada ya hapo miili itarudishwa nyumbani kwa ajili ya maziko.