Meya Moshi atajwa kesi ya Sabaya

Meya Moshi atajwa kesi ya Sabaya

Muktasari:

  • Shahidi wa nne katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, Hajirin Saad Hajirin (32) ameieleza mahakama kuwa Diwani wa Sombetini (CCM), Bakari Msangi wakati anapigwa alimmomba Sabaya amsamehe kwa sababu ni ndugu wa rafiki yake Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu Juma.

Arusha. Shahidi wa nne katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, Hajirin Saad Hajirin (32) ameieleza mahakama kuwa Diwani wa Sombetini (CCM), Bakari Msangi wakati anapigwa alimmomba Sabaya amsamehe kwa sababu ni ndugu wa rafiki yake Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu Juma.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo, shahidi huyo alisema alipata kipigo kikali kutoka kwa aliodai ni mabaunsa wa Sabaya hivyo diwani akawa anaomba asamehewe.

Katika kesi hiyo, Sabaya ameshtakiwa na wenzake wawili ambao ni Sylvester Nyegu na Daniel Mbura.

Shahidi alisema Msangi aliendelea kupigwa kwa muda wa nusu saa na akamweleza Sabaya kuwa mdogo wake ambaye ni meya wa Moshi (ila hakumbuki jina), ni rafiki yake (Sabaya).

Mbali na kupigwa kwa amri ya Sabaya, alisema watu hao walikuwa na bastola ambayo kuna wakati aliishika Sabaya na wakati mwingine waliishika mabaunsa wake. Sehemu ya mahojiano kati ya shahidi huyo na wakili Chavula yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili: Eeh baada ya kumweleza maneno hayo nini kilitokea?

Shahidi: Sabaya aliamuru mabaunsa wamtoe mahabusu Bakari.

Wakili: Shahidi baada ya kutoa maelekezo hayo nini kilitokea?

Shahidi: Walimkamata na kuanza kumpiga makofi usoni na kwenye masikio walisimama kwa nyuma wakampigisha magoti,

Wakili: Nini alichokifanya huyo Bakari?

Shahidi: Akaanza kupigwa huku akilia akiuliza anapigwa kwa kosa gani, Sabaya anaamrisha wamtoe mahabusu wakaendelea.

Wakili: Shahidi hebu ieleze mahakama ukiacha kitendo cha kumpiga huyo Bakari, nini kingine walichomfanyia?

Shahidi: Kabla ya kupigwa alipekuliwa.

Wakili: Alipekuliwa kwa maelekezo ya nani?

Shahidi: Alipekuliwa na mabaunsa kwa maelekezo ya DC Sabaya.

Wakili: Shahidi hebu tuambie ulishuhudia wakichukua vitu gani kutoka kwa Bakari.

Shahidi: Walichukua simu na wallet

Wakili: Shahidi hebu tuendelee baada ya kumpiga Bakari nini kiliendelea?

Shahidi: Alipopata nafasi Bakari alimrukia DC Sabaya kwenye mguu, akamwambia unanishika? Muondoe huyu. Akamwambia “Mheshimiwa, mke wangu anaumwa.”

Wakili: Aliposema mkewe mgonjwa nini kilitokea?

Shahidi: Waliendelea kumpiga kichwani akaendelea kupiga kelele na kila alipoendelea kupiga kelele ndivyo alivyoendelea kupigwa.

Wakili: Shahidi hebu tueleze vipigo hivyo kwa Bakari viliendelea kwa muda gani?

Shahidi: Alipigwa kwa zaidi ya nusu saa.

Wakili: Hebu ieleze mahakama huyo DC Sabaya na hao wenzake alioshirikiana nao walikuwa wana vitu gani wamebeba?

Shahidi: Kulikuwa na bastola nyeusi ambayo mwanzo aliishika DC Sabaya na baadaye niliona mabaunsa wake walikuwa wanaishika, walikuwa na redio call ambayo nadhani walikuwa wakiwasiliana na magari ya nje

Wakili: Shahidi hebu tuambie sasa wewe kwa upande wako ulipata madhila gani?

Shahidi: Kuna muda ulifika wa kufungua saumu kwa sababu nilikuwa nimefunga nikaomba maji ya kunywa lakini sikupewa, nikawa natabasamu mmoja wao akasema mheshimiwa huyu anacheka anafanya anacheka inaonekana anaona hili jambo siyo serious.

Wakili: Shahidi hebu tuambie huyo aliyokuwa amezungumza maneno hayo unaweza ukaieleza mahakama mwonekano wake ukoje?

Shahidi: Alikuwa mpana wa wastani,siyo mrefu sana wala sio mfupi

Imeandaliwa na Mussa Juma na Janeth Mushi.