Mfanyabiashara ashauri uhakiki eneo la biashara za baa, kumbi za starehe

Muktasari:

  • Ofisa Mtendaji wa Baa na kumbi ya Starehe ya Soweto Pazuri Park, iliyopo jijini Dar es Salaam, Sekela Mwaihabi ametupia lawama Serikali uamuzi wa kufungia maeneo hayo ya biashara za starehe bila kuhakiki wa eneo husika la biashara hizo.

Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji wa Baa na kumbi ya Starehe ya Soweto Pazuri Park, iliyopo jijini Dar es Salaam, Sekela Mwaihabi ametupia lawama Serikali juu ya uamuzi wa kufungia maeneo hayo ya biashara za starehe bila kuhakiki wa eneo husika la biashara hizo.

 Mwaihabi amesema alifungua biashara hiyo kwa kibali bila pingamizi lolote kutoka serikalini kuhusu mazingira ya biashara yake, akishauri kuanzia sasa mamlaka husika zihakiki eneo la biashara kabla ya kumpatia kibali cha biashara ili kuepuka usumbufu na hasara wanazoingia wakati wa biashara.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Mei 10, 2023 wakati wa mjadala unaotafuta suluhisho la fungia fungia kumbi za starehe kwa sababu ya kelele chini ya Jukwaa la Mwananchi twitter space, linaloandaliwa kila Jumatano.

Mjadala huo unaakisi uamuzi wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kufungia jumla ya baa na kumbi za starehe 89 baada ya kupiga kelele na mitetemo iliyozidi viwango husika.

“Mimi nadhani mlipa kodi yeyote anapotaka kufungua biashara basi Serikali ikahakiki eneo husika kama lina sifa, kwa mfano baa nimefungua Agosti mwaka jana lakini baadaye wakafungia biashara yangu, walikuja zaidi ya mara nne wanasema muziki wa kawaida,” amesema

“Lakini baadaye wanakuletea barua unapiga mziki mkubwa, nikiomba kibali cha bendi nazuiliwa, usiku wakija polisi nachukuliwa, ilinikatisha tamaa sana, ikabidi nipunguze wafanyabiashara ili kuepuka hasara, kwa hivyo mtu akiomba kibali, aambiwe kabisa wewe huruhusiwi kufanya biashara eneo hilo.”

Katika mjadala huo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samuel Gwamaka amesema, “tumefikia hatua hii baada ya kupata malalamiko ya kelele kwa wananchi kwani watu hawalali, ndani ya miaka mitano tumepata barua nyingi.”

“Kwa mkoa wa Dar es Salaam, tuliitisha kikao na wamiliki wa baa na kumbi za starehe kuwaelimisha kuhusu madhara ya kelele. Tuliendelea kutoa elimu hadi ngazi za manispaa kutoa elimu kwa viuongozi wa kata hadi mitaa,” amesema

Mkurugenzi huyo amesema kabla ya kumfungia mhusika, hufanya vikao na mashauriano lakini, “kama unavyojua sikio la kufa halisikia dawa, ndio maana kilichowakuta ndio hawa 89 na mchakato unaendelea, ndio maana baadhi yao wameandika barua ya kukiri makosa na wengi wameandika na kulipa faini.”