Mhariri Mwananchi ashauri mbinu mpya kudhibiti kelele baa, kumbi za starehe

Muktasari:

  • Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imeendesha mjadala wa TwitterSpace ikiwa na mada ‘kufungia baa, kumbi za starehe kwa sababu ya kelele ni suluhisho”, na kushirikisha wadau mbalimbali.

Dar es Salaam. Kaimu Mhariri wa maudhui ya Biashara, Gazeti la Mwananchi, Ephraimu Bahemu amesema wafanyabiashara wanatakiwa kujenga utamaduni wa kudhibiti kelele zinazozidi kiwango mitaani badala ya kuendelea kuishi kwa kuogopa sheria za nchi.

 Bahemu aliyeshauri busara itumike katika adhabu hizo akisema mamlaka husika kwenda mbali zaidi katika udhibiti wa kelele, akihusisha kelele za magari barabarani na maeneo mengine.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Mei 10, 2023 wakati wa mjadala unaotafuta suluhisho la fungia fungia kumbi za starehe kwa sababu ya kelele chini ya Jukwaa la Mwananchi twitter space, linaloandaliwa kila Jumatano.

Mjadala huo unaakisi uamuzi wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kufungia jumla ya baa na kumbi za starehe 89 baada ya kupiga kelele na mitetemo iliyozidi viwango husika.

“Nafikiri busara itumike ili kurejesha shughuli zao ili biashara zisiathirike. Lakini pia, kelele zipo nyingi katika mazingira, hiyo ni bugdha kwa wengine, magari barabarani, kwa hiyo udhibiti unatakiwa kwenda mbali zaidi,” amesema Bahemu.

“Ndio maana mataifa mengine ya nje inakuwa nadra kusikia kelele nje, ukipiga kelele wengine wanakushanga, inabidi tujenge utamaduni, ila watu wajenge utamadunia na siyo kuogopa sheria.”

Katika hatua nyingine, Bahemu ametupia lawama wafanyabiashara kutozingatia agizo hilo lililokuwa na maelekezo ya NEMC kwa muda mrefu,“ilikuwa ni busara kwa mfanyabiashara kupima mwenyewe kiwango cha kelele ili kuepuka adhabu ya kufungiwa.”

“Kwa hiyo wanafanyabiashara waliteleza kwa upande wao pia, walipaswa kuwajibika. Unanunua kipimo kile na kupima sauti yako, hata NEMC wakija unatoa ushahidi wa kipimo cha kelele zako,” amesema Bahemu.”

Bahemu amesema, “udhibiti wa kelele unapaswa kwenda katika maeneo tofauti, lakini pia hili jambo linapaswa kwenda taratibu na watu kuelimishwa.”

Akigusia suala la ajira amesema, “lakini katika maeneo hayo, kuna watu wameajiriwa huku sehemu kumbi ni wasafirishaji wakiwemo bodaboda wanaosubiri abiria nje ya maeneo ya baa au kumbi za starehe kuwapeleka maeneo mbalimbali.”