Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mfuko NHIF unavyotafunwa na magonjwa yasiyoambukiza

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akizungumza katika mkutano wake na vyombo vya habari jijini Dodoma uliolenga kujibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa kuhusu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)

Muktasari:

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa mchanganuo wa namna ambavyo magonjwa yasiyoambukiza yanautafuna Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) akieleza kuwa fedha zilizotumika kugharamia magonjwa hayo mwaka 2014/15 imeongezeka maradufu.

Dar es Salaam. Siku chache baada ya taarifa za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kudaiwa kuwa na dalili za kufa kutokana na kuelemewa matibabu na madeni ya wanachama Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametaja kiasi cha fedha kinachotumika kugharamia magonjwa yasiyoambukiza.

Waziri Ummy ametoa takwimu hizo leo Alhamisi, Septemba Mosi, 2022 katika mkutano wake na vyombo vya habari jijini Dodoma uliolenga kujibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa kuhusu Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Ametoa angalizo akisema nchi inashuhudia ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza huku mfuko huo ukiwa katika hatari ya kuelemewa na mzigo wa magonjwa hayo kwa rasilimali fedha na watu ikiwemo saratani, magonjwa ya moyo, figo na mengine.

“Gharama za kuhudumia wagonjwa wanaopatiwa tiba ya kemikali dawa na mionzi kwa mwaka 2015/16 Sh9 bilioni na mwaka 2021/22 tunalipia Sh22.5 bilioni hili haliendani na ongezeko la wanachama wa NHIF,” amesema.

Amesema huduma za matibabu ya figo tumetoka zilitumia Sh9.5 bilioni lakini kwa mwaka 2021/22 zimetumika Sh35.42 bilioni ambapo ilitoka idadi ya wagonjwa 280 na sasa wamefikia wagonjwa 2099.

Waziri aanika chanzo mfuko NHIF kuyumba

“Ukiangalia gharama za matibabu ya moyo zililipwa Sh500 milioni kwa mwaka 2015/16 sasa hivi bilioni 4.35 zinatumika na vipimo vya CT Scan na MRI vimeongezeka kutoka malipo ya Sh5.43 hadi kufikia Sh10.89 bilioni kwa mwaka 2021/22,” amesema.

Waziri Ummy ametoa angalizo katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza huku akitaja vitu vitatu ambavyo Watanzania wanapaswa kujiepusha navyo ikiwemo sukari, chumvi na mafuta.

NHIF ilitumia jumla ya Sh99.09 bilioni kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kulipia huduma zilizotolewa kwa wagonjwa wanaougua magonjwa yasiyoambukiza.

“Dawa za saratani zinakula zaidi mfuko wa NHIF ukiangalia haya ni magonjwa yanayotokana na mtindo wa maisha, magonjwa mengine ni pamoja na huduma ya kusafishwa damu kwa wagonjwa wa figo dialysis tunatumia Sh35.4 bilioni kwa mwaka,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bernald Konga.