Serikali yawekwa kitanzini mzigo wa madeni NHIF

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya kujadili jinsi ya kudhibiti ugonjwa wa kipindupidu iliyoandaliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kuzishirikisha nchi za ukanda wa Afika Mashariki na Kati na Kusini uliofanyika jijini Dar es salaam juzi. Na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

  • Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeitaka Serikali kuacha kulalamika kuhusu kulegalega kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na badala yake itoe suluhisho kwa kuharakisha muswada wa bima ya afya kwa wote Bungeni, wakitaja ndiyo mwarobaini wa tatizo hilo.


Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeitaka Serikali kuacha kulalamika kuhusu kulegalega kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na badala yake itoe suluhisho kwa kuharakisha muswada wa bima ya afya kwa wote Bungeni, wakitaja ndiyo mwarobaini wa tatizo hilo.

Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tangu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipobainisha dalili za kufa kwa mfuko huo kutokana na kuelemewa na madeni ya matibabu ya wanachama wake huku akiyataja magonjwa sugu kuwa chanzo.

Aidha, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ya mashirika ya umma ya Machi 2022 inaonyesha NHIF ilipata hasara ya Sh109.71 bilioni.

NHIF pia inaidai Serikali kiasi cha Sh30.4 bilioni pamoja na mkopo usio na mkataba wa kiasi cha Sh129.04 bilioni, fedha ambazo zilichukuliwa na Serikali kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, kwa mujibu wa ripoti ya CAG.

Akizungumza jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Stanslaus Nyongo alisema kwa hali ilivyo kama mfuko utabaki ulivyo utakufa na kwamba kamati hiyo imekuwa ikitoa mapendekezo yake mara kwa mara nini kifanyike kwa wizara ya afya.

“Serikali haitakiwi kulalamika, ije na suluhisho, tulishasema kwenye kamati mwarobaini wake ni kuwa na bima kwa watu wote maana yake tukiwa na bima ya aina hiyo mfuko utaimarika kifedha, watakaotoa fedha ni watu wazima hawaumwi hivyo utakuwa na nguvu,” alisema.

Alisema kwa kuwa makusanyo ni madogo na matumizi makubwa mfuko unazidiwa, “Suluhisho tukienda kwenye sheria ya bima ya watu wote kutakuwa na ulazima wa sheria kila mtu atachangia fedha, wadau watachangia, wananchi wa kawaida, makampuni yatachangia utaimarika kifedha na utahudumia wateja wake vizuri.”

Akitolea mfano, Nyongo alisema mtu mmoja anachangia kiasi cha Sh100 na anatumia Sh170 au Sh200, hali inayochangia kuzorota kwa uhai wa mfuko.

Aliitaka NHIF kuunda mifumo mizuri ili kudhibiti matumizi kwa wateja na watoa huduma kuuibia mfuko, kwani bila kufanya hivyo mfuko huo hautakuwa na maisha marefu.

Nyongo alisema nyenzo nyingine ni kuhakikisha watu wanajiepusha na magonjwa yasiyoambukiza na kwamba elimu itolewe ili kuwanusuru wananchi, kwani ndiyo chanzo cha mfuko kuelemewa. “Magonjwa ya moyo, kisukari, figo ni magonjwa ambayo watu wanakunywa dawa maisha yao yote.”

Alipoulizwa kuhusu kusuasua kwa muswada wa bima ya afya, Nyongo ambaye ni Mbunge wa Maswa Mashariki (CCM) alisema mpaka sasa Serikali haijasema ugumu uko wapi. “Kila siku wanasema wataleta, hawaleti hawajasema sababu ni nini ili na sisi tutoe maoni yetu.”

Juzi, akifungua mkutano wa siku tano wa kikanda wa kuwajengea uwezo kuhusu ugonjwa wa kipindupindu jijini Dar es Salaam, Waziri Ummy alitaja magonjwa yasiyoambukiza ndiyo sababu kuu ya gharama kubwa.

Magonjwa yasiyoambukiza yanajumuisha moyo, saratani, mfumo wa upumuaji na kisukari yanayochangia asilimia 71 ya vifo vinavyotokea duniani ambapo ni sawa na watu milioni 41 kila mwaka.

Akisisitiza kuhusu uelewa wa dalili za magonjwa na jinsi ya kujikinga nayo, Waziri Ummy alisema “fanyeni kuwa jukumu la msingi ili kuzuia kuenea kwa maambukizi, najua tutafanikiwa kupambana na kipindupindu katika nchi zetu.”

Kutokana na hali hiyo, waziri huyo ameiagiza NHIF kuachana na utaratibu iliouanzisha hivi karibuni wa kudhibiti idadi ya wagonjwa wanaohudhuria vituo vya afya.

Aidha, Agosti 25 mwaka huu, Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) ilisema, imebaini mfuko huo kwa sasa unatengeneza nakisi katika mapato na matumizi, jambo ambalo linatishia uhai wa mfuko.

Mwenyekiti wa PIC, Jerry Silaa alisema baada ya kupokea taarifa ya uwekezaji na hesabu za mfuko huo na kufanyia uchambuzi, kamati imeelekeza NHIF kufanya mchakato kwa kuongeza wanachama kwa sababu malipo ya huduma za wanachama yamekuwa yakiongezeka ukilinganisha na mapato yanavyoongezeka.

“Kwa hiyo gharama zinaongezeka kuliko mapato na hii inahatarisha uhai wa mfuko, kwa hivyo kamati imeelekeza ifanye juhudi za makusudi za kuongeza wanachama,” alisema Silaa.

Pia, aliuagiza mfuko huo kuwa na jitihada za makusudi za kuhakikisha kuna utaratibu mzuri wa kudhibiti matumizi, kuboresha mifumo ya Tehama ili kupunguza udanganyifu na kuongeza mapato.

Mbali na hayo, NHIF ilitumia Sh99.09 bilioni kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 kwa ajili ya kulipia huduma zilizotolewa kwa wagonjwa wanaougua magonjwa yasiyoambukiza.

Fedha hizo ni sawa na asilimia 18 ya fedha zote ambazo zililipiwa katika kushughulikia magonjwa sugu, huku dawa za saratani na huduma ya kusafishwa figo ‘dialysis’ zikitumia fedha nyingi zaidi.

“Dawa za saratani zinakula zaidi mfuko wa NHIF, ukiangalia haya ni magonjwa yanayotokana na mtindo wa maisha, magonjwa mengine ni pamoja na huduma ya kusafishwa damu kwa wagonjwa wa figo, dialysis tunatumia Sh35.4 bilioni kwa mwaka,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernald Konga.


Madeni ya Serikali

Katika ripoti yake ya 2020/21 CAG, Charles Kichere alisema kwenye mapitio yake katika mfuko huo alibaini kukua kwa gharama za mafao kwa kasi kuliko ongezeko la mapato ya michango kwa miaka mitano iliyopita.

Alisema hiyo ilisababisha nakisi ya Sh59.03 bilioni mwaka 2020/21, hali inayohatarisha ukwasi wa mfuko na uwezo wake wa kujiendesha.

“Nilibaini kutokuwapo kwa usimamizi wa mikopo yenye thamani ya Sh209.70 bilioni inayotolewa na NHIF kwa taasisi za Serikali ambapo kiasi cha Sh79.47 bilioni kilikuwa kimeiva lakini hakikukusanywa hadi Juni 30, 2021.”

“Mfuko unakabiliwa na upotevu wa fedha kutokana na kuongezeka kwa hatari ya kutorejeshwa kwa mapato na changamoto za mtiririko wa fedha kutokana na deni kubwa ambalo halijakusanywa.” Alisema na kuongeza kuwa alibaini mikopo ya Sh98.47 bilioni iliyoiva ambayo haijalipwa.

“Nilibaini kuwa mfuko haukuwa na mkataba uliotiwa saini kwa ajili ya mkopo wenye thamani ya Sh129.04 bilioni uliotolewa kuanzia mwaka wa fedha 2010/11 hadi 2020/21 kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa na ununuzi wa vifaatiba vya hospitali hiyo,” alisema Mdhibiti.

CAG alisema NHIF ilikuwa ikiidai Serikali kiasi cha Sh30.4 bilioni kama fedha za kibiashara na Sh4.5 iliidai sekta binafsi.