Mtikisiko NHIF wazua hofu nchini

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya kujadili jinsi ya kudhibiti ugonjwa wa kipindupidu iliyoandaliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kuzishirikisha nchi za ukanda wa Afika Mashariki na Kati na Kusini uliofanyika jijini Dar es salaam juzi. Na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

  • Wakati mikakati ya kuboresha huduma za afya ikiendelea kuwekwa, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amebainisha dalili za kufa kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutokana na kulemewa na madeni ya matibabu ya wanachama wake.

Dar es Salaam. Wakati mikakati ya kuboresha huduma za afya ikiendelea kuwekwa, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amebainisha dalili za kufa kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutokana na kulemewa na madeni ya matibabu ya wanachama wake.

Akifungua mkutano wa siku tano wa kikanda wa kuwajengea uwezo kuhusu ugonjwa wa kipindupindu jijini hapa jana, Waziri Ummy alitaja magonjwa yasiyoambukiza ndiyo sababu kuu ya gharama kubwa.

“Kuongeza uelewa ni jambo la msingi, kwa mfano bima yetu ya afya (NHIF) inakaribia kufa kwa kuwa umeelemewa na ongezeko la madai yanayohusu NCD (magonjwa yasiyoambukiza),” alionya Ummy.

Magonjwa yasiyoambukiza yanajumuisha moyo, saratani, mfumo wa upumuaji na kisukari yanayochangia asilimia 71 ya vifo vinavyotokea duniani ambapo ni sawa na watu milioni 41 kila mwaka.

Akisisitiza kuhusu uelewa wa dalili za magonjwa na jinsi ya kujikinga nayo, Waziri Ummy alisema “fanyeni kuwa jukumu la msingi ili kuzuia kuenea kwa maambukizi, najua tutafanikiwa kupambana na kipindupindu katika nchi zetu.”

Kutokana na hali hiyo, waziri huyo ameiagiza NHIF kuachana na utaratibu iliouanzisha hivi karibuni wa kudhibiti idadi ya wagonjwa wanaohudhuria vituo vya afya.

Katika taarifa yake aliyoitoa hivi karibuni, Waziri Ummy alisema licha ya dhamira njema ya mfuko huo kuondoa uovu unaofanywa na wamiliki wa vituo vya afya, wanapaswa kukaa na wadau kukubaliana njia ya kuchukua.

Hata hivyo, bado NHIF inadai kuna udanganyifu mkubwa unaofanywa na watoa huduma kwenye vipimo kwa magonjwa.


Kamati ya Bunge

Wiki iliyopita, Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) ilisema imebaini matumizi makubwa kwenye gharama za huduma za wanachama wa NHIF, hali inayotishia uhai wa mfuko huo.

Hayo yalibainishwa baada ya kamati hiyo kujadiliana na NHIF kuhusu taarifa za uwekezaji na hesabu za mwaka wa fedha 2020/2021.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, Jerry Silaa alisema kutokana na hali hiyo, kamati imeishauri NHIF kuandaa mkakati wa kuongeza wanachama zaidi.

“Baada ya kujadiliana tumekuja na maelekezo matatu ikiwamo kuutaka mfuko kuja na mpango wa kuongeza idadi ya wanachama kwa sababu hesabu zake zimeonyesha matumizi ni makubwa kwa maana ya malipo ya huduma za wanachama yanazidi kuongezeka ukilinganisha na mapato wanayokusanya, hii inahatarisha uhai wa mfuko,” alisema Silaa.

Mwenyekiti huyo alisema kamati imeuagiza mfuko kuwa na jitihada za makusudi za kuweka utaratibu mzuri wa kudhibiti matumizi.

Alisema wameutaka kuimarisha mifumo ya Tehama kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma sambamba na kudhibiti mianya ya udanganyifu.


Ushauri kuiokoa NIHF

Akizungumzia na Mwananchi kwa simu jana, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Shedrack Mwaibambe, alisema ili kuunusuru mfuko huo, Serikali inapaswa kupunguza wigo wa NHIF na kuanzisha mifuko mingine miwili ambayo itakayochukua watu kulingana na hali zao.

Dk Mwaibambe alisema kwa hali inavyoendelea ni wazi mfuko huo umeelemewa na idadi kubwa ya watu ambao mchango wao hauendani na huduma zinazotolewa.

Kutokana na hilo, alishauri licha ya NHIF, uanzishwe mifuko mingine itakayohudumia sekta isiyo rasmi na wasio watumishi wa umma.

“Sasa hivi wigo umeongezeka, wanachama ni wengi na ukifuatilia kwa karibu, utagundua wanaotumia zaidi huduma za matibabu ni wazee na watoto ambao matibabu yao ni ghali,” alisema.

Ukiwapo mfuko wa watumishi wa sekta binafsi watakaohudumiwa kwa utaratibu tofauti na wa sekta isiyo rasmi nao ukawahudumie wastaafu, watoto, bodaboda na watu wenye shughuli zisizo rasmi, alisema kutakuwa na ufanisi tofautina ilivyo sasa.

Dk Mwaibambe pia alishauri kuanzishwa kwa mfumo utakaomtambua mhusika anayeenda kutibiwa na kadi ya NHIF.

“Uwepo mfumo wa biometric, inaweza kuwa gharama lakini utasaidia kukabiliana na udanganyifu. Hii ina maana ili mnufaika atibiwe itatakiwa aweke kidole kujithibitisha maana kuna udanganyifu mwingi unafanyika kwenye huu mfuko,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi Tanzania (Aphta), Dk Egina Makwabe, alisema ili kunusuru mfuko huo lazima Serikali iangalie upya gharama za vifurushi ili kupunguza wengi kutegemea michango ya wachache.

Dk Makwabe pia alisisitiza siasa zisiingizwe kwenye afya badala yake ukweli uwekwe wazi.

“Ukiangalia hivi vifurushi mfano cha watoto ambacho gharama yake ni Sh50,400 kwa mwaka, bado ni kidogo. Tukumbuke katika kundi ambalo linatibiwa zaidi ni watoto sasa kama anatibiwa mara nyingi gharama za matibabu zinakuwa juu, huyu lazima atatumia fedha za wachangiaji wengine, itanyonya mfuko. Nashauri waangalie hivi vifurushi na waweke udhibiti kuhakikisha hakuna udanganyifu. Kingine, Serikali iruhusu uchangiaji gharama kwa baadhi ya huduma zilizo ghali sana,” alisema.

Makwabe alisema mabadiliko ya gharama ni suala ambalo limekuwa likijadiliwa kwa miaka mingi bila kupata mwafaka na NHIF imeendelea kutumia bei za mwaka 2016 licha ya mabadiliko yaliyotokea.

“Suala la bei ni sugu, bei ambazo watoa huduma binafsi tunazozitumia na za serikalini zilitolewa mara ya mwisho mwaka 2016 sasa hivi ni mwaka 2022 ni miaka sita na bei haijawahi kubadilika. Kuna bei zimeshuka na nyingine zimepanda kutokana na maisha yalivyo,” alisema.

Alitolea mfano bei ya dawa ya panado kwamba hununuliwa kati ya Sh35 hadi Sh250 kwa kidonge kutegemea na ilikotoka lakini NHIF itamlipa mtoa huduma ni Sh20. Iwapo mtoa huduma ataitoa dawa hiyo, alisema atafanya hivyo kwa hasara na mwisho wa siku vituo vitadorora kiuchumi na kushindwa kulipa kodi hata mishahara ya wafanyakazi.


Taarifa ya NHIF

Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 11 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema wametumia Sh99.09 bilioni mwaka 2021/22 kulipia magonjwa yasiyoambukiza.

Alisema kiasi hicho ni sawa na asilimia 18 ya fedha zote zilizolipwa huku dawa za saratani na huduma ya kusafishwa figo (dialysis) zikitumia fedha nyingi zaidi. Alisema magonjwa yasiyoambukiza ni mzigo mkubwa kwa mfuko huo.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga

“Dawa za saratani zinaila zaidi NHIF. Haya ni magonjwa yanayotokana na mtindo wa maisha, kuna huduma ya kusafishwa damu kwa wagonjwa wa figo, tunatumia Sh35.4 bilioni kwa mwaka,” alisema.

Konga, alisema mpaka sasa mfuko huo una wanachama 4,831,233 sawa na asilimia nane ya Watanzania wote huku asilimia sita wakihudumiwa na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) huduma nyingine za bima zikihudumia asilimia moja. Hata hivyo, alisema kuna udanganyifu mwingi unaofanywa na watoa huduma hali inayouumiza mfuko huo lakini wanapambana na hali hiyo.

“Udanganyifu upo na tumekuwa tukichukua hatua, tutasitisha mikataba itakayoonekana inahatarisha uendelevu wa mfuko. Tumekuwa tukichukua hatua ikiwamo kupiga faini, kuwaripoti wahusika katika mabaraza yao kuhakikisha tumelipia huduma halali kulingana na miongozo,” alisema Konga.

Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mashirika ya umma ya Machi 2022, inaonyesha NHIF ilipata hasara ya Sh109.71 bilioni.


Wananchi watahadharisha

Christopher Wana, mkazi wa Temeke alisema gharama za matibabu ni ghali na endepo hakutakuwa na bima Watanzania wengi watatumia mitishamba.

“Ugonjwa wowote matibabu yake yapo juu, kwa vipato vyetu hivi hatuwezi kumudu kujitibu hasa magonjwa haya ya kisukari au presha, ni muhimu kwa Serikali kuiwezesha NHIF ili huduma ziwe endelevu kwa wananchi, tukisikia mfuko umekufa maana yake wananchi ndio tumekufa,” alisema.

Naye Suzana Andrew, wanachama wa NHIF mkoani Geita alisema “hivi majuzi nilienda hospitalini lakini nikaambiwa dawa nikanunue, hali ikiendelea hivi, sisi wenye kipato cha chini tutaumia. Hakuna mbadala wa maisha, ukikosa huduma unakufa. Rais aangalie hili la NHIF kwa umakini mkubwa.”

Warda Anthony, mkazi wa Kigamboni alisema NHIF ni mkombozi wa wananchi wengi hasa wasiomudu gharama za matibabu.

Imeandikwa na Dickson Ng’hily, Elizabeth Edward na Baraka Loshilaa.