Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mgodi wa Mwadui waanza uzalishaji ukitangaza hasara ya Sh149 bilioni

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme akizindua mtambo wa uzalishaji katika mgodi wa Williamson Diamond. Picha na Suzy Butondo

Muktasari:

Kuanza kwa uzalishaji mgodini kumefanyika baada ya marekebisho na ujenzi wa bwawa la takatope na malipo ya fidia kwa wananchi kutoka viji vya Ng’wanholo na Nyenze vilivyoko Kata ya Mwadui Lohumbo Wilaya ya Kishapu walioathirika na topetaka iliyoharibu siyo tu mashamba, bali pia nyumba na mali kadhaa ikiwemo samani za ndani.

Shinyanga. Mgodi wa Almasi wa Williamson Diamond Mwadui umeanza tena uzalishaji baada ya kusitisha shughuli kwa takriban miezi tisa baada ya bwawa la topetaka kupasuka na kuingia kwenye mashamba na makazi ya watu.

Kurejea kwa uzalishaji katika mgodi huo ni utekelezaji wa agizo la Juni 30, 2023 lililotolewa na Waziri wa Madini, Dotto Biteko kwa uongozi wa mgodi huo kuwezesha Serikali Kuu, halmashauri na jamii inayozunguka mgodi kunufaika kupitia mapato.

Hafla ya kuanzisha shughuli za uzalishaji mgodini hapo ziliongozwa Julai 17, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme huku Meneja Mkuu wa Williamson Mwadui, Ayoub Mwenda akisema kusitishwa kwa shughuli hizo tangu Novemba 11, 2022 kumesababisha hasara ya zaidi ya Sh149 bilioni.

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu huyo, hasara hiyo imetokana na kupoteza uzalishaji wa kati ya kareti 25, 000 hadi 30, 000 za almasi iliyokuwa ikizalishwa kwa mwezi. Kareti moja ya almasi katika soko la dunia ni Dola za Kimarekani 270.

“Hasara hiyo pia imeathiri hadi mapato ya halmashauri kupitia kodi na ushuru mbalimbali bila kusahahu utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia miradi ya uwajibikaji kwa jamii inayotegemea uzalishaji na mapato ya mgodi,’’ amesema Mwenda

Fidia kwa waathirika

Kuanza kwa uzalishaji mgodini kumefanyika baada ya marekebisho na ujenzi wa bwawa la takatope na malipo ya fidia kwa wananchi kutoka viji vya Ng’wanholo na Nyenze vilivyoko Kata ya Mwadui Lohumbo Wilaya ya Kishapu walioathirika na topetaka iliyoharibu siyo tu mashamba, bali pia nyumba na mali kadhaa ikiwemo samani za ndani.

Ofisa Mahusiano wa Williamson Diamond Mwadui, Benard Mihayo amesema zaidi ya Sh1.8 bilioni zimetumika kuwalipa fidia wananchi 294 kati ya 304 walioathirika na topetaka kutoka mgodini huku watu sita malipo yao yakisubiri maelewano kati ya wanafamilia kuhusu nani apokee malipo.

"Fidia hiyo inahusisha fedha taslimu na mali na samani za ndani zilizoharibiwa. Pia tutawajengea waathirika nyumba katika maeneo mapya salama yaliyotengwa na Serikali,’’ amesema Mihayo

Charles Mang'ombe, mkazi wa Kata ya Mwadui Luhumbo aliyeathiriwa na topetaka ameishukuru Serikali kwa kusimamia haki ya malipo ya fidia, wajibu wa kujenga upya bwawa la topetaka na kuruhusu mgodi huo kuwanza uzalishaji akisema siyo tu utarejesha na kuimarisha mzunguka wa fedha na shughuli za kiuchumi Kishapu, bali pia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia fedha za uwajibikaji kwa umma, CSR.

Akifungua shuguli za uzalishaji mgodini hapo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme aliupongeza uongozi wa Williamson Diamond Mwadui kwa kutekeleza kwa ufasaha maagizo ya Serikali ya kujenga upya bwawa la topetaka na kurejesha uzalishaji.

"Jengeni bwawa jingine la akiba ili kujiweka tayari siyo tu hili jipya likijaa, bali pia dharura yoyote napotokea. Pia pandeni miti kuzunguka bwawa la takatope kuongeza uimara wa kingo, kutunza na kulinda mazingira,’’ aliagiza RC Mndeme

Mbunge wa Kishapu, Boniface Butondo ameunga mkono hoja ya uongozi wa mgodi kuimarisha kingo za bwawa kuepusha wananchi na madhara kama iliyoshuhudiwa Novemba, 2022 bwawa la topetaka lilipopasuka na matope kujaa kwenye mashamba na makazi ya wananchi.