Mgombea CCM ajinadi ananguvu za kiume

Wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wa CCM, Wilaya ya Dodoma. Picha na Habel Chidawali

Muktasari:

  • Mgombea wa nafasi ya mjumbe wa halmashauri ya CCM wilaya ya Dodoma amewavunja mbavu wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya baada ya kuwaomba wamchague kwa sababu ana nguvu za kiume.Dodoma. Mgombea wa nafasi ya mjumbe wa halmashauri ya CCM wilaya ya Dodoma amewavunja mbavu wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya baada ya kuwaomba wamchague kwa sababu ana nguvu za kiume.

Mgombe huyo, Chris Madaha ametoa kauli hiyo leo Oktoba Mosi, 2022 wakati akiomba kura mbele ya wajumbe 1,344 walioshiriki mkutano huo katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma.

Madaha ambaye aliomba kura kupitia kundi la vijana, amesema amekamilika kwa sehemu zote na ana nguvu za aina mbili ambazo ni za kimwili na kiume.

“Ndugu wajumbe, mimi nimepewa namba mbili ambayo ni namba ya ushindi, lakini nina nguvu za aina mbili ambazo ni nguvu za kimwili na kiume, nipeni kura zetu,” amesema Madaha.

Kauli hiyo ilisababisha vicheko vya wajumbe na kusababisha zogo lakini waliponyamaza aliyarudia maneno yake mara mbili.

Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni mkuu wa wilaya hiyo, Jabir Shekimweri alimuomba mgombea kipaza sauti na kumtaka akapumzike wakati watu wakiendelea kucheka.

Uchaguzi wa CCM wilaya ulihusisha nafasi ya mwenyekiti, wajumbe wa mkutano mkuu wa taifa, mkutano wa mkoa na wajumbe wa halmashauri kupitia makundi ya wazazi, vijana na wanawake.