Mgomo ulivyowanufaisha wasafirishaji mizigo, huduma yarejea

Daladala zikiendelea na utoaji wa huduma ya usafirishaji wa abiria jijini Mwanza.

Muktasari:

 Licha ya kurejea kwa huduma ya usafirishaji kwa njia ya daladala, baadhi ya wadau wa sekta ya usafirishaji wameishauri Serikali kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa hoja zilizosababisha mgomo

Mwanza. Vita vya panzi furaha ya kunguru ndivyo unavyoweza kusema baada ya madereva wa bajaji za kusafirishia mizigo kuchangamkia fursa ya kusafirisha abiria jijini Mwanza, wenzao wa daladala wakigoma juzi kutoa huduma hiyo.

Kutokana na mgomo huo uliolenga kushinikiza kuondolewa bajaji katika njia za daladala, baadhi ya wakazi wa Jiji la Mwanza walilazimika kupanda bajaji za mizigo walizotozwa kati ya Sh2,000 hadi Sh3, 000 kulingana na umbali huku walioshindwa kumudu gharama hiyo wakilazimika kutembea kwa miguu.

“Kikawaida huwa napata Sh30,000 kwa siku kwa kubeba mizigo hapa Buhongwa, siku nyingine kazi inakuwa ngumu naweza hata kupata Sh15,000 lakini ikitiki nalaza hata 50,000 lakini jana (juzi) mgomo ulivyotokea kwakweli nililala na zaidi ya Sh3000,000,”amesema Juma Mrisho dereva wa bajaji ya mizigo

Amesema japo hakutumia shida ya usafiri kama njia ya kujipatia kipato ilimlazimu kuwatoza abiria Sh2,000 kwa kila mmoja kuwafikisha kituo chochote wanachoshuka na mwisho wa safari yake ilikuwa stendi ya posta.

“Nilipiga trip zaidi ya 15, kwenda mjini na kurudi Buhongwa na kila trip nilibeba abiria zaidi ya 10. Kwakweli ilikuwa siku ya neema kwetu japo abiria walipata shida lakini kwetu tuliingiza pesa,”amesema.


Abiria wazungumza

Justina Edwin, mfanyabiashara wa duka la nguo Mtaa wa Lumumba jijini Mwanza amesema mgomo huo si tu uliwasababishia kutumia bajeti kubwa ya nauli lakini pia uliwachelewesha kazini na kuwafanya kupitia purukushani nyingi hadi kupata usafiri.

“Mbaya zaidi walichagua siku ya kugoma Jumatatu siku ambayo inakuwa na watu wengi wenye uhitaji wa usafiri. Walitufanya tukawa kama mizigo kwenye makenta na bajaji za mizigo maana tulikuwa tunagombania, kusukumana ilimradi tupate nafasi hata kwa kurundikana kwakweli jana tuliteseka sana,”amesema Justina.

Abiria mwingine, Iddi Matti amesema anaamini kwenye biashara huria, kwakuwa abiria ni wengi ikilinganishwa na daladala zinazofanya kazi Mwanza.

“Abiria bado ni wengi usafiri ni changamoto ukitaka bajaji zifungiwe sidhani kama ni sahihi maana zinarahisisha usafiri, sehemu ambazo bajaji zinafanya kazi ni sehemu ambazo bado zinahitaji daladala kuongezeka. Hadi watu kupanda bajaji ambayo ni gharama kubwa kuliko daladala ina maana wana shida kubwa ya usafiri,”anasema.


Wadau washauri Serikali

Licha ya kurejea kwa huduma ya usafirishaji kwa njia ya daladala, baadhi ya wadau wa sekta ya usafirishaji wameishauri Serikali kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa hoja zilizosababisha mgomo kuepusha hali hiyo kujirudia siku zijazo.

Mdau wa masuala ya kijamii, Mwanaidi Omari ameitaka Serikali kushugulikia hoja na changamoto zinazopelekwa mezani na kuzitatua mapema kabla uamuzi kama migomo haujaamuliwa kuwaondolea adha wananchi.

“Naishukuru Serikali ya Mkoa wa Mwanza maana ilitatua changamoto ya mgomo wa daladala japo asubuhi tuliteseka sana, naishauri iangalie namna nzuri ya kupanga bajaji kwa sababu ni Watanzania wenzetu ambao wanatafuta riziki na wenyewe wakipewa nafasi ya kufuata utaratibu sioni sababu ya kuondolewa barabarani,”amesema.


Msimamo wa wamiliki, madereva daladala

Akizungumzia mgomo huo ulioisha jana jioni baada ya majadiliano na makubaliano kati ya watoa huduma na Serikali na Chama cha wamiliki wa daladala Mkoa wa Mwanza (MTA), Mjumbe wa MTA, Kamugisha Amos amesema walirudi barabarani juzi jioni baada ya kukubaliana kuundwa kwa kamati itakayofanya kazi siku saba kushugulikia malalamiko yao.

“Kabla ya mgomo tuliishaomba changamoto ya bajaji kuingilia kazi za daladala itatuliwe lakini kwakuwa utekelezaji unakuwa mdogo tukaamua kusitisha huduma huenda wakalifanyia kazi kwa haraka, haiwezekani tangu mwaka 2020 malalamiko yetu ni yaleyale,”amesema

Kuhusu hasara waliyoipata wamiliki wa daladala ya kukusa Sh80,000 kwa siku kwa magari aina ya Coaster na Sh50,000 kwa Hiace.

Dereva wa daladala njia ya Nyamadoke - Nyashishi, Emmanuel Ibrahim amesema endapo madai yao hayatatatuliwa ndani ya muda walioahidiwa watagoma tena kushinikiza yatatuliwe.


Serikali yaahidi kutatua ndani ya wiki mbili

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagaa, Amina Makilagi na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala  amesema waliahidi kutatua changamoto hiyo ndani ya wiki mbili kama ambavyo zilipendekezwa na watoa huduma hiyo.

Makilagi amesema tayari imeundwa kamati yenye wajumbe 30 ili kufanya ufuatiliaji wa kina kuhusu suala hilo.

“Utaratibu wote wa kutambua vituo na kila kitu tutakuwa tumefanya, ninyi nendeni na sisi tuendelee kufanya kazi, huduma zote ziendelee kufanya kazi kwa utaratibu baada ya wiki mbili tutakuwa tumekaa vizuri.”