Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mgomo wa daladala waisha lakini...

Muktasari:

  • Baada ya kufanya mgomo kwa siku mbili mfululizo na kurejea tena barabarani jana, madereva wa daladala wa jijini hapa wanalalama wakidai Serikali imewageuzia kibao kuhusiana na madai yao.

Arusha. Baada ya kufanya mgomo kwa siku mbili mfululizo na kurejea tena barabarani jana, madereva wa daladala wa jijini hapa wanalalama wakidai Serikali imewageuzia kibao kuhusiana na madai yao.

Mgomo huo ambao sasa ni mara ya tatu kufanyika jijini humo, ulianza Agosti 14, ukihusisha wamiliki wa daladala kukishinikiza pikipiki za matairi matatu, maarufu bajaji kuondolewa kwenye ruti wanazofanya kazi kwa madai zinawabeba abiria wao.

“Yaani mimi nashangaa Serikali imetugeuka, tuligoma ili kushinikiza bajaji ziondolewe mjini kwenye ruti tunazofanya kazi, lakini leo (jana) nashangaa tunaondolewa sisi wanaendelea na kazi wao, kiukweli hapa Serikali haijatutendea haki,” alidai John Issaka, dereva wa njia ya Moshono.

Hata hivyo, Mwananchi lilizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa kuhusiana na kauli hiyo ambapo alisema yote yanayofanyika ni makubaliano waliyokaa wajumbe wa kamati ya kushughulikia mgogoro huo, ulioitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela.

“Nani anasema tumewageuzia kibao wakati huu ni utekelezaji wa mapendekezo ya kamati iliyoundwa na mkuu wa mkoa baada ya mgomo wao wa Julai tatu, (mwaka huu), na uzuri wao walikuwa wajumbe wengi zaidi na wakaafiki kuondolewa bajaji katika ruti hizo na wakapendekeza eneo la kuhamishia stendi ile iwe hapa eneo la Fire,” alisema Mtahengerwa.

Alisema katika moja ya vikao waliwataarifu wajumbe hao kuwa lile eneo la stendi, Serikali inatarajia kujenga soko la kisasa na madereva daladala wakapendekeza stendi ihamishiwe eneo la wazi la Fire na ndicho kinachofanyika.

Alisema hivi sasa wanaendelea kuboresha eneo hilo la stendi mpya kwa kujenga miundombinu ya vyoo, jana waliomba waendelee kuegesha magari stendi ya zamani, ombi lililokubaliwa.

Alisema kuanzia leo daladala zote zitapakia na kushusha abiria eneo hilo.

Wakati mkuu huyo wa wilaya akisema hayo, Katibu mwenezi wa umoja wa madereva daladala, Mussa Njuga alisema kauli za kugeukageuka zinazotolewa na viongozi wa Serikali zinawaweka katika wakati mgumu viongozi wa madereva hao.

“Yaani dada yangu hapa nimechoka kabisa, kwa sababu tuliomba bajaji ziondolewe na tulikubaliana jana (juzi) na maofisa wa polisi wa mkoa na wilaya kuwa watafanya msako hivyo tuhamasishe wanachama wetu warudi kazini, leo (jana) inakuja kauli nyingine.

“Wanachama wanalalamika na sisi viongozi tumechoka kuhangaika, tunashindwa hadi kufanya kazi nyingine, tunasikilizia kinachofanywa ili tuchukue hatua zaidi,” alisema.

Naye dereva Joseph Mollel anayeegesha daladala inayoelekea kwa Mrombo, alisema juzi walikubaliana na viongozi wao kusitisha mgomo baada ya kuelezwa kuwa madai yao yanafanyiwa kazi, ikiwemo uhakiki wa bajaji na kuziondoa, lakini jana wanashangaa bado zipo na wao ndio wanaotakiwa kuondoka katikati ya mji.

"Mimi ruti yangu ninakwenda kwa Mrombo, awali nilikuwa napita mjini Soko la Kilombero hadi Stendi ndogo, lakini leo maaskari wamejaa mjini wanatulazimisha tupande na njia ya Esso, kwenda Hospitali ya NSK hadi soko la Samunge na kugeuzia mzunguko wa Fire, kule hakuna abiria na ni mbali,” alilalama dereva huyo.

Akilifafanua hilo, Ofisa Mfawishi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) Mkoa wa Arusha, Joseph Michael alisema mpaka sasa wameshahakiki bajaji 749 na zimepangwa katika vituo 38 jijini humo na eneo la Arumeru, huku kila kituo kikitakiwa kuwa na bajaji 30 tu.

“Tumemaliza uhakiki na tumewapanga kwenye vituo tumezingatia uhai wa leseni, lakini pia walipokuwa wakiegesha awali, hivyo kinachofuata ni kuwasomea tu wakae kwenye maeneo yao wafanye kazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za leseni zinavyowaelekeza,” alisema Michael.

Alisema bajaji zilizokuwa hazina leseni watazipangia utaratibu wa usajili na kuzielekeza katika maeneo mengine ambayo bado kuna uhaba wa usafiri kutokana na mahitaji.

“Arusha ni kubwa, hasa katika wilaya nyingine, hivyo hawa watakaobaki hatutawatelekeza, bali tutawapangia utaratibu mzuri wa kuhakikisha wanaendelea na kazi, hivyo kuanzia sasa tunaomba kila mmoja afuate sheria na utaratibu wake wa kazi,” alisisitiza.

Naye Makamu Mwenyekiti wa umoja wa madereva wa bajaji wilaya ya Arusha, Shafii Andalo alisema wamepokea mapendekezo hayo na wanatarajia kuitisha mkutano mkuu ili kuwaeleza wanachama wao kuhusu ruti mpya walizopangiwa.