Mhudumu akimbia uvamizi, zahanati ya kijiji yafungwa

Muktasari:

Zahanati ya Kijiji cha Ikonya katika Kata ya Bara wilayani Mbozi, mkoani Songwe imefungwa tangu Juni 2, 2022 baada ya mhudumu kuvamiwa na mtu aliyeingia kwenye makazi yake na kumpora simu tatu na kompyuta mpakato.

Songwe. Zahanati ya Kijiji cha Ikonya katika Kata ya Bara wilayani Mbozi, mkoani Songwe imefungwa tangu Juni 2, 2022 baada ya mhudumu kuvamiwa na mtu aliyeingia kwenye makazi yake na kumpora simu tatu na kompyuta mpakato.

Akisimulia tukio hilo, Esther Chitete, mhudumu wa zahanati hiyo, alisema tukio hilo lilitokea Juni 1, mwaka huu majira ya saa 2 za usiku akiwa nyumbani kwake, huku amefunga geti lakini mlango wa sebuleni ukiwa wazi.

“Nikiwa napika, binti yangu wa kazi alikuwa sebuleni, ghafla mtu aliingia akiwa amefunika sura kwa barakoa na kubakiza macho tu. Alituamuru tulale chini, aliuliza hela ziko wapi, nikamwambia sina hela,” alisema Esther.

Alisema mtu huyo alipekua mikoba na mabegi na kisha alichukua mkoba mmoja aliobebea laptop na simu tatu.

“Wakati akiendelea kupekua nilipata upenyo nikataka nitoroke lakini aliniwahi akanikamata na kunipiga sana.

“Alisema ametumwa kuniua lakini kwa kuwa ni mjamzito ameamua kuniacha, hivyo akashauri nihame eneo hilo akidai waliomtuma watatuma mtu mwingine,” alisema.

Alidai kuwa mvamizi pia alitaka kuwabaka yeye na binti yake lakini walipiga kelele akatokomea.

“Binti yangu alimdanganya kuwa fedha zipo chumba cha pili ndipo alipokwenda kuzitafuta, tukapata nafasi ya kupaza sauti zaidi ili majirani wasikie, ndipo jambazi huyo aliondoka,” alisema Esther.

Baadaye walipiga simu polisi huku wanakijiji wakimsaka mhusika bila mafanikio.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikonya, Mateso Zyenje alisema zahanati hiyo ilikuwa na wahudumu wawili, lakini mmojawapo, Elibariki Chakula, yupo masomoni na kubaki Esther.

Zyenje ameiomba Serikali kuwasaidia wapate mhudumu mwingine kwa kuwa wananchi zaidi ya 6,000 na wengine wa vijiji jirani wanaitegemea.

Magdalena Mkea, mmoja wa wanakiijiji, alisema zahanati hiyo ilikuwa ikiwasaidia sana, hasa kwa huduma za mama na mtoto hivyo kufungwa kwake kumeleta kero ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma.