Miili miwili ya walioangukiwa na ukuta yazikwa Dar

Muktasari:

Mingine miwili yasafirishwa kwa maziko Kigoma

Dar es Salaam. Miili ya watu wawili kati ya wanne wa familia moja waliofariki dunia kwa kuangukiwa na ukuta wa nyumba waliyokuwa wakiishi imezikwa.

Ajali hiyo ilitokea Mtaa wa Goroka B, Toangoma, mkoani Dar es Salaam.

Miili mingine imesafirishwa kwenda mkoani Kigoma.

Ajali ilitokea asubuhi ya Aprili 26, 2024. Waliofariki dunia ni Lidya Heza (21), Agnes Eliya (20), Stella Rujukundi (20) na Joyce Rujukundi (12).

Ukuta ulibomoka wakiwa wamelala kwenye chumba kimoja. Katika ajali hiyo mmoja alinusurika.

Ajali hiyo ilisababishwa na nyumba ya jirani kuathiriwa na mvua hivyo matofali kuporomoka na kuangukia ukuta. Pamoja na matofali kulikuwa na maporomoko ya tope.

Miili iliyosafirishwa kwenda Kigoma ni ya Lidya na Agnes, waliokuwa wamefika Dar es Salaam kumjulia hali mama yao mdogo Mariamu Julius aliyekuwa mgonjwa.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 28, 2024 Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Goroka B, Ntinyahela Lutayaba amesema miili hiyo imesafirishwa kwa gari kwenda Kigoma.

“Ratiba ilianza asubuhi tulienda kuchukua miili yote mochawari katika Hospitali ya Rufaa ya Polisi ya Kilwa Road,” amesema.

Amesema mili iliyozikwa Dar es Salaam ni ya watoto wa Mariamu wa kuwazaa ambao ni Stella na Joyce. Wamezikwa Kata ya Toangoma, mtaa wa Masaki.

Akizungumza na Mwananchi jana Aprili 27, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda amesema Serikali imetoa baadhi ya gharama za kuendesha shughuli za msiba huo.

"Kama Serikali tumetoa majeneza yote manne na tumetoa ubani kidogo wa kusaidia shughuli ya mazishi," amesema Sixtus