Mikoa minane kupata mvua kubwa leo usiku

Muktasari:

  • Wakati Msemaji wa Serikali Mobhare Matinyi akitangaza vifo vya watu 33 vilivyotokana na athari za mvua mkoa wa Pwani na Morogoro kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa angalizo ya mvua kubwa mikoa nane usiku wa leo.

Dar es Salaam. Kuanzia leo saa 3:00 usiku, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mikoa nane itashuhudia mvua kubwa.

 Mikoa hiyo ambayo maeneo machache yatashuhudia mvua kubwa ni Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Lindi, Mtwara, Pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Taarifa hiyo ya TMA imetolewa leo Aprili 12, 2024 na tayari mamlaka hiyo imeshatabiri uwepo wa mvua kubwa kwa mikoa 14 kwa siku tano kuanzia jana.

“Upepo mkali unaozidi kasi ya km 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayozidi mita mbili vinatarajiwa kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi Mkoa wa Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Lindi, Mtwara na visiwa vya Unguja na Pemba,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, TMA imetoa angalizo ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo machache ya mikoa ya Njombe na Ruvuma

Ikumbukwe, Aprili 10, TMA ilieleza kuwa mikoa 14,  Mkoa wa Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Pwani Lindi, Mtwara, Rukwa, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe, Ruvuma na visiwa vya Unguja na Pemba vitashuhudia vipindi vya mvua leo Aprili 12, 2024.

Aprili 13, TMA imetaja mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Morogoro, Pwani, Lindi na Mtwara pamoja na Unguja na Pemba kushuhudia mvua kubwa.

“Baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Iringa, Njombe na Ruvuma nazo zitapaswa kuchukua tahadhari kwani mvua kubwa inatarajiwa kunyesha,” imeeleza taarifa hiyo juzi.

Akizungumza leo na waandishi wa habari, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mobhare Matinyi amesema kwa taarifa ya Jeshi la Polisi Aprili mosi hadi  Aprili 11, watu 19 wamepoteza maisha kutokana na  kutokana na mvua kubwa zinazonyesha maeneo mbalimbali nchini.

Mikoa aliyotaja kutokea kwa vifo hivyo ni Lindi, Njombe, Tanga, Pwani (Mkuranga na Kibaha), Manyara, Mbeya, Geita na Rukwa.

Mbali na hayo, kwa mkoa wa Pwani na Morogoro pekee alisema mvua hizo zimesababisha vifo vya watu 33  vifo 28  mkoa wa Morogoro na vitano Mkoa wa Pwani, huku mali na miundombinu ya makazi, barabara shule, hospitali na mazao ya chakula vikiathirika vibaya.