Mikoa minne kujua maeneo reli itakapopita

Muktasari:
Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema linafanya tathimini katika mikoa minne nchini itakayowasilishwa kwa wadau wa mikoa hiyo itakayoelezea maeneo itapita reli, lengo likiwa ni kuepuka bomoa bomoa.
Dodoma. Shirika la Reli Tanzania (TRC) linafanya tathimini katika mikoa minne ikiwemo Dodoma ili kufahamu maeneo itakapopita reli, lengo ni kuepuka bomoa bomoa.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi Agosti 6, 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa wakati akizungumzia utekelezaji wa shughuli na bajeti ya mwaka 2022/2023.
Kadogosa ametaja mikoa hiyo ni pamoja na Arusha, Mbeya, Mwanza na Dodoma ambapo wiki ijayo watakuwa wanawasilisha kwa wadau.
“Nafikiri wiki inayokuja tutakuwa na uwasilishaji hapa kwa ajili ya tathimini iliyofanyika wadau wote watakusanyika wafanyiwe presentation,” amesema.
Amesema wanafanya tathimini hiyo kabla ya watu hawajawa wengi Dodoma ambayo itasababisha kubomoa nyumba za watu wengi.
“Tunataka reli ijulikane kabisa imepita wapi hapa Dodoma, Mji Arusha, Mwanza na Mbeya tunafikiri lazima kuwe na reli,” amesema.
Pia, amesema baada ya uwekezaji uliofanyika wa reli ya kawaida sasa usafirishaji mizigo umeongezeka kutoka tani 186, 833 kabla ya mabadiliko hadi tani 417,380 Juni 2021 ikiwa ni sawa na asilimia 232.
Kuhusu mradi wa reli ya kisasa wa SGR, Kadogosa amesema thamani ya uwekezaji wa ujenzi wa reli hiyo umefikia Sh 16 trilioni kwa awamu ya kwanza ya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
“Serikali hadi sasa imelipa malipo yote yenye jumla ya Sh6.4 trilioni ya malipo ya kazi yote iliyotelekezwa na kuhakikiwa ubora wake,” amesema.
Aidha, Kadogosa alisema mradi huo umetoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania wapatao 16,000 na ajira zisizo rasmi kwa zaidi ya watu 80,000.