Mirembe: Magonjwa ya zinaa husababisha matatizo afya ya akili

Muktasari:

  • Asema ugonjwa huo unatabia ya kutoisha kabisa badala yake unakwenda kwenye mfumo wa fahamu na kubaki katika eneo hilo kwa muda mrefu.

Iringa. Imeelezwa kuwa Magonjwa ya zinaa ikiwemo kaswende yanachangia kwa kiasi fulani kupata ugonjwa wa Afya ya akili huku akiwasisitiza wataalam kuwafuatilia na kuwachunguza Magonjwa hayo hasa ya ngono.

Hayo yamebainishwa na Daktari bingwa wa afya ya akili, Mfumo wa fahamu kutoka Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili – Mirembe, Dk Damas Andrea, ambapo amesema kuwa ugonjwa huo unatabia ya kutoisha kabisa na badala yake unakwenda kwenye mfumo wa fahamu na kubaki katika eneo hilo kwa muda mrefu.

"Kama ulipata ugonjwa wa kaswende ukiwa na umri wa miaka 20 ukafikiri umepona, lakini kwa bahati mbaya unakwenda kwenye mfumo wa fahamu kisha unaibuka ukiwa na umri wa miaka 35 mpaka 60 ndio unajitokeza kwa njia ya aina nyingine ikiwemo changamoto ya kupoteza kumbukumbu, kuona au kusikia vitu ambavyo havipo," amesema.

Dk Andrea amesisitiza kwamba ugonjwa huo unatibika hivyo mgonjwa ambaye atagundulika inamsaidia kupata matibabu na kurudi katika hali yake ya kawaida bila shida yoyote.

Pia Dk Andrea ametaja magonjwa mengine yanayoweza kusababisha afya ya akili kuwa ni ugonjwa wa ukimwi huku akisema kwa sasa Wizara ya Afya inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha vituo vya kutokea huduma za matibabu ya ukimwi, pia huduma ya afya ya akili inatolewa.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospital ya Rufaa Mkoa wa Iringa, Dk Alfred Mwakalebela, ameishukuru timu ya wataalum kutoka katika taasisi hiyo kwa utaalam ambao wameutoa kwa wataalum wa hospitali hiyo.

Timu hiyo kutoka Mirembe imepiga kambi ya siku nne katika hospital hiyo ya ya rufaa na kufanikiwa kuhudumia jumla ya wagonjwa 205.