Miti shamba, teknolojia na imani potofu vyatajwa tatizo la macho

Daktari kutoka Kitengo cha Pua, Koo na Sikio (ENT) katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dk Titus Kansio akimpima mkazi wa Mwanza mfumo pua, sikio na macho wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye ulemavu ambapo Bugando ilitoa vipimo hivyo bila malipo. Watu 80 kati ya 160 waliopimwa walikutwa na matatizo ya macho huku Zaidi ya nusu wakiwa ni watoto. Picha na Mgongo Kaitira.
Muktasari:
Watu milioni 3 nchini, sawa na asilimia 3.3 ya watu milioni 60 kwa mujibu wa Senza ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 wana ulemavu wa aina mbalimbali ikiwemo ulemavu wa macho, jambo linaloongeza umuhimu wa jamii kuchukua hatua dhidi ya mambo yanayoweza kusababisha ulemavu yakiwemo maradhi.
Mwanza. Wakati wazazi na walezi wakishauriwa kujenga utamaduni wa kuchunguza uwezo wa kuona wa watoto wao kubaini mapema matatizo ya macho kabla hayajafika hatua mbaya, matumizi ya dawa za miti shamba, imani potofu na matumizi yasiyo sahihi ya maendeleo ya teknolojia yametajwa kuwa miongoni mwa vyanzo vya matatizo ya macho nchini.
Wito huo umetolewa leo Jumanne Desemba 5, 2023, na Daktari Bingwa Bobezi wa mifupa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Dk Inyas Akaro wakati maadhimisho ya siku ya kimataifa ya ‘Watu wenye ulemavu’ yaliyofanyika jijini Mwanza.
Dk Akaro amesema kati ya watu 160 waliofanyiwa vipimo mbalimbali mwilini kwa siku mbili hospitalini hapo, watu 80 sawa na asilimia 50 wana matatizo ya macho huku robo ya wanaoumwa matatizo hayo wakiwa ni watoto.
Daktari huyo amesema uchunguzi huo umebaini idadi kubwa ya watoto walipatwa matatizo hayo wakati wa kuzaliwa na wengine kupata majeraha wakati wa makuzi yao.
“Unaweza kuwa unatoa maelekezo kwa mtoto wako halafu hatekelezi jambo linalopelekea ufikirie kuwa amekudharau kumbe haoni ama kusikia maelekezo unayompatia. Tuna wajibu wa kuwachunguza mara kwa mara,” amesema Dk Akaro.
Kuhusu visababishi, Dk Akaro ametaja ajali, ulemavu wakati wa makuzi, matumizi holela ya miti shamba, teknolojia na imani potofu kuchangia watu wengi kuugua matatizo hayo huku wengine wakiishia kupata upofu.
“Kuna wenye matatizo ya macho yanayosababishwa na umri, Tracoma, presha ya macho, mtoto wa macho. Pia robo ya watoto waliozaliwa na matatizo ya macho na walikuwa nyumbani bila kupatiwa matibabu,” amesema
Mkurugenzi Mkuu wa Bugando, Dk Fabian Massaga amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha watu bilioni 1.3 sawa na asilimia 16 ya watu wote duniani wana ulemavu wa aina mbalimbali ikiwemo wa macho.
Kwa hapa nchini, Dk Massaga amesema watu milioni tatu kati ya milioni 60 sawa na asilimia 3.3 wana ulemavu wa aina mbalimbali ikiwemo ulemavu wa macho jambo ambalo linaonyesha kuwa jamii inatakiwa kuchukua hatua dhidi ya maradhi hayo.
“Katika jamii tuna watu wenye ulemavu unaoonekana na usiyoonekana, tunapaswa kufuatilia watu wanaotuzunguka ili tusije kuwatendea visivyo kwa kudhani wako sawa kumbe wana ulemavu na wanahitaji msaada wetu,” amesema Dk Massaga
Mkazi wa Nyasaka jijini Mwanza, Happiness Machira ameishukuru Bugando kwa kutoa vipimo hivyo bila malipo huku akiiomba kufikisha huduma hiyo maeneo ya vijijini kwa kile alichodai huduma hizo hazifiki.
“Tunashukuru kwa sababu tumetibiwa bure leo lakini tutafurahi zaidi endapo jamii hasa maeneo ambayo hawawezi kufika hapa Bugando kwa urahisi ikifikiwa na kupatiwa elimu, tutaweza kutokomeza magonjwa yanayoweza kuepukika,” amesema Machira.
Katika kuadhimisha siku ya ‘Watu wenye ulemavu duniani,’ Bugando imetoa huduma ya vipimo vya magonjwa ya mfumo wa sikio, pua, koo (ENT), magonjwa ya mifupa na magonjwa yasiyoambukiza bila malipo kwa siku mbili kuanzia jana Desemba 4, mwaka huu.