Mjamzito afariki duniani kwa kushambuliwa na mamba akioga ziwani

Muktasari:
- Salome Senge (28) mkazi wa Kijiji cha Nyambeba, Kitongoji cha Kazunzu wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza amefariki dunia kwa kwa kushambuliwa na mamba wakati akioga Ziwa Victoria.
Buchosa. Salome Senge (28) mkazi wa Kijiji cha Nyambeba, Kitongoji cha Kazunzu wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza amefariki dunia kwa kwa kushambuliwa na mamba wakati akioga Ziwa Victoria.
Tukio hilo limetokea Machi 24, 2023 saa moja jioni, ambapo mama huyo alikwenda kuoga na alikutana na dhahama ya kushambuliwa na mamba.
Ofisa Mtendaji Kata ya Kazunzu, Tabitha Marwa amethibitisha kutoka kwa tukio na mabaki ya mwili wake yamepatika huku baadhi ya viongozi vya mwili havionekana kutokana na kuliwa na mamba.
"Ni tukio la kuhuzunisha na kusikitishwa, mama huyo mjamzito aliyeshambuliwa na mamba alikuwa nakaribia kujifungua hivyo imeleta simanzi kutokana na matarajio ya kupata mtoto kutoweka,” amesema.
Salome Sange amekuwa mtu wa nane kushambuliwa na mamba kwa kipindi cha miezi mitatu mwaka huu 2023.
Pia mkazi wa Kijiji cha Kanoni Kisiwa cha Maisome alishambuliwa na mamba na kufariki dunia na kuacha watoto sita wakiwa yatima, huku watu wengine sita wakipoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba kwenye Kisiwa Kome wilayani humo.
Licha ya elimu iliyotolewa na Idara ya Wanyamapori kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na madhara ya kushambuliwa na mamba, wamekuwa na mazoea ya kupuuza elimu hiyo.
Paul Seke ni mjomba wa marehemu amesema tukio hili ni pigo kubwa kwa familia yao, huku akitoa wito kwa jamii kuacha mazoea ya kuoga ziwani, badala yake wanatakiwa kuteka maji na kuoga nyumba hii itakuwa njia pekee ya kuepuka madhara ya kushambuliwa na mamba.
Idara ya Wanyamapori ikiongozwa na Ofisa Msaidizi, Mohamed Mpoto ilikuwa imepiga kambi wilayani Sengerema hususani Halmashauri ya Buchosa kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na madhara ya kushambuliwa mamba.
Baadhi ya wananchi wameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu na kujenga vizimba vya kuzui wananchi kushambuliwa na mamba wakati wakifanya shughuli mbalimbali za kijamii ndani ya Ziwa Victoria.