Mkakati wa Serikali kupunguza madhara ya kupikia kuni, mkaa

Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza katika mahojiano maalumu na wahariri wa Mwananchi leo Oktoba 25, 2022.

Muktasari:

Mara ngapi umewahi kujiuliza madhara yaliyomo kwenye moshi unaotokana na kupikia nishati ya kuni na mkaa kwa afya yako? Wataalamu wanasema kupikia nishati ya kuni kwa saa moja ni sawa na mtu aliyevuta sigara 300.

Dar es Salaam. Unafahamu kuwa kitendo cha kuwemo jikoni kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara 300 kama unapikia nishati ya kuni au mkaa?

Si hivyo tu, takriban watu 33,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na kutumia nishati chafu ya kupikia, ikiwemo kuni, mkaa, mabaki ya mazao na kinyesi cha wanyama.

Nishati hizo kwa mujibu wa mtaalamu wa magonjwa ya upumuaji, Dk Elisha Osati, zinazalisha kemikali ya monoksidi ya kaboni inayoathiri oksijeni kwenye seli mwilini.

Kama ulidhani hatari za kiafya na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya upumuaji yanasababishwa na hewa pekee umekosea, nishati chafu ya kupikia ni chanzo kingine cha majanga hayo.

Kulingana na wataalamu watu milioni 38.8 wanaishi wakiwa na magonjwa yanayotokana na matumizi ya nishati hizo, yaliyopo katika mfumo tofauti.

Waziri wa Nishati, January Makamba katika mahojiano maalumu na wahariri wa Mwananchi leo Oktoba 25, 2022, amesema athari za matumizi ya nishati chafu ya kupikia huku akieleza kuhusu kampeni ya nishati safi ya kupikia itakayozinduliwa Novemba 1-2, 2022.

“Asilimia 80 ya nishati yetu inatumika nyumbani kwa ajili ya kupikia, ukiangalia wanapikaje utakuta wengi wao wanatumia nishati chafu ambazo ni kuni, mkaa, mabaki ya mazao na vinyesi vya wanyama,” amesema Makamba.

Hata hivyo, Makamba ameeleza athari katika matumizi ya nishati hiyo hazipo katika afya pekee, bali kijamii na uchumi.

Kwa mujibu wa Makamba, wanawake hasa vijijini hutumia saa nne hadi tano kutafuta kuni, hivyo wanakutana na majanga mbalimbali ikiwemo kubakwa.

Makamba amesema katika mkutano huo kuhusu nishati safi ya kupikia zitashuhudiwa shuhuda za wanawake wahanga wa pilikapilika za kusaka nishati, wakiwemo ambao wamekutana na unyanyasaji wa kingono wakiwa porini huku wanafunzi wakishindwa kusoma kwa utulivu.

Hata hivyo, amesema katika mkutano huo Rais Samia Suluhu Hassan atatoa muelekeo wa Serikali yake kuhusu nishati safi ya kupikia.

“Nina imani kubwa na utekelezaji wa mpango huu ambao ni mtambuka na unahusisha wizara na wadau kutokana wizara na sekta mbalimbali nchini.

“Tunataka kuokoa wananchi wetu dhidi ya janga hili ambalo halizungumzwi sana, lakini ni hatari. Kila nyumba inahitaji nishati safi ya kupikia hivyo, katika kutekeleza sera za wizara yangu, hili la nishati safi ya kupikia ni miongoni mwa majukumu yangu ya msingi.

“Kongamano hilo litatupa mwanga wa wapi kwa kuanzia, utekelezaji wa mikakati mbalimbali ikiwemo kutafuta fedha za kufanikisha kuwawezesha watanzania angalia asilimia 70 kutumia nishati safi ya kupikia,” amesema Makamba.


Walichokisema wadau wa afya

Akisisitiza kuhusu madhara ya matumizi ya nishati ya kuni na mkaa, Dk Osati alisema: “Kwa mfano umefungiwa sehemu kuna jiko la mkaa unawaka unatoa moshi ingawa wengi hatuuoni ule moshi unazunguka na kuleta hilo tatizo kuna matukio ya watu wengi kufa.”

Ameyataja madhara ya muda mrefu kuwa ni watu kupata ugonjwa wa ‘Pulmonary COPD’ unaosababisha kikohozi, mafua na maumivu kwenye mapafu.

“Yaani mishipa ya njia ya hewa ndogondogo inatanuka mtu anashindwa kupata hewa vizuri, imehusianishwa sana na wanaotumia kuni na mkaa COPD ni magonjwa ya mapafu yanayosababisha mirija ya hewa kushindwa kutanuka na kushindwa kubeba hewa vizuri,” amesema.

Amesema ugonjwa huo wanaopata aghalabu hushindwa kuiruhusu hewa kuingia kwa kuwa ndani ya mirija hujaa majimaji.

Wengine, amesema huwa na dalili za pumu ikiwemo kukohoa mara kwa mara, “Waathirika ni wengi na vifo vingi pia. Tunawatibu hawa wagonjwa na ikitokea anapona anakuwa na makovu kwenye mapafu yake na mishipa kushindwa kurudi kwa wakati,” amesema Dk Osati.

Kemikali hiyo inaharibu maafu moja kwa moja, iwapo nishati hizo zitatumika kwa muda mrefu, kama anavyoeleza Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Alex Masao.

“Kuni sumu yake inakua juu zaidi kwa kuwa moshi unaotoka unakua zaidi na Carbon dioxide inayosababisha damu kushindwa kusafirishwa kwenye oksijeni na hivyo kukata pumzi,” amesema.

Kiwango cha kemikali, amesema kinatokana na moto uliowashwa, akisisitiza kuwa anayenunua mkaa na kuutumia sehemu iliyofungwa ikiwemo kwenye banda au ndani ya nyumba athari yake ni kubwa zaidi.

Dk Masao amesema muda wa matumizi ndiyo unaozalisha madhara kwa mtumiaji kwani kwa siku chache ni vigumu kuona madhara kwa kuwa moshi huwa na chembechembe tofauti ambazo zinaenda kukaa kwenye mapafu.

Hatari si kwa upumuaji pekee, hata macho ni shida, Daktari bingwa wa magonjwa ya macho kutoka Hospitali ya Taifa Mloganzila, Anna Sanyiwa amesema machozi yanayosababishwa na moshi yakiendelea husababisha macho kuywa mekundu.

Amesema kiwango cha athari hutofautiana kulingana na mti unaotumika kama kuni, akifafanua ipo inayosababisha muwasho mkali na mingine kidogo.

Takwimu za ulimwengu

Kulingana na utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO), moshi unaotokana na kuni za kupikia ni mojawapo ya visababishi vikuu vya vifo vya watoto wachanga duniani, vikigharimu maisha ya watoto 500,000 chini ya miaka mitano kila mwaka.

Utafiti huo unachambua matumizi ya nishati hizo na kuenea kwa magonjwa ya kupumua kwa watoto hao kupitia tafiti 41 zilizofanywa katika nchi 30 zinazoendelea kutoka bara la Asia, Afrika na Amerika ya Kusini.

Matokeo yalipendekeza jamii kuweka nje majiko yanayotumia nishati hizo ambapo tafiti zinaonyesha takriban watu bilioni tatu katika nchi zinazoendelea wanategemea kuni au mkaa kwa ajili ya kupikia.

Kwa mujibu wa WHO magonjwa yanayosababishwa na moshi husababisha vifo vya watu milioni 4.3 kila mwaka vikiupiku ugonjwa wa Malaria na kifua kikuu.