Mke wa Rugemalira asimulia miaka minne ilivyokuwa ‘giza’

Rugemalira: sijawahi nyoa nywele, mke wake amshukuru Rais, Paroko aishangaa imani yake

Muktasari:

  • Mke wa mfanyabiashara James Rugemalira, Benedicta Rugemalira amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya awamu ya sita kwa kumuachia huru mume wake, hatua aliyosema imeoindoa familia yake kwenye giza.


Dar es Salaam. Mke wa mfanyabiashara James Rugemalira, Benedicta Rugemalira amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya awamu ya sita kwa kumuachia huru mume wake, hatua aliyosema imeoindoa familia yake kwenye giza.

Amesema kipindi cha miaka minne ambacho mume wake alikaa gerezani ilikuwa ni giza kwa familia, kwa kuwa walikuwa hawaelewi kama ipo siku mfanyabiashara huyo atakuwa huru kutokana na msimamo alioweka.

Benedicta aliyeambatana na mumewe, alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni muda mfupi baada ya kutoa sadaka ya shukrani wakati wa azimisho la misa takatifu iliyofanyika katika Parokia Katoliki ya Makongo Juu.

“Tulikuwa hatuelewi cha kufanya, maana wapo waliokuwa wanasema akubali alipe hizo fedha ili atoke, lakini mwenyewe alisimama imara na kusema hawezi kusema uongo na yuko tayari kwa lolote kuthibitisha ukweli wake.

“Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kumwezesha Mzee Rugemalira kutoka gerezani, ukweli ni kwamba tulikuwa kwenye giza zito, ila waumini mmekuwa na sisi kuanzia kwenda kumtembelea gerezani hata kuungana nasi kwenye maombi yaliyotuwezesha kuvuka kitanzi hiki,” alisema Benedicta na kuongeza:

“Shukrani za pekee ziende kwa baba paroko, nimekuwa nikimbilia kwake kila wakati pale ninapokuwa na kitu chochote kilichonishika rohoni, amekuwa akinitia moyo na kunipa maneno ya kunifariji . Si hivyo tu, mara kadhaa alikuwa akienda gerezani kumfariji mzee.”

Paroko wa parokia hiyo, Padri Joseph Massenge aliwasihi waumini kuiga mfano wa Rugemalira wa kuwa imara na kusimamia kile anachokiamini kwa kuwa hivyo ndivyo Ukristo unataka.

Alisema siku zote anayesimamia ukweli Mungu anamsaidia na kumuinua kwenye magumu anayopitia, alisema huku akisisitiza “kusimamia haki na ukweli ulio safi.”

“Mnatakiwa kuiga mfano wa maisha haya, jitoe sadaka simamia ukweli. Kama unasimamia ukweli, hivyo hivyo hata kama utakufa, simamia ukweli. Kuna watu wengi wanateseka wanafanyiwa vitu vya ajabu, wewe simamia ukweli.

“Mzee nakupongeza umesimamia ukweli mpaka dakika ya mwisho na hivyo ndivyo Mungu anataka. Mungu anamjalia yule anayesimama katika haki na haya ndiyo maisha tunayotakiwa. Hata katika mambo madogo, simamia haki na ukweli Mungu atakuimarisha na kukuongoza.

Alisema, “Huyu mzee anastahili kuingia kwenye kile kitabu cha Guiness kutokana na msimamo alioonyesha, huu ndio Ukristo wa kweli. Mama amenifuata mara nyingi kuniambia nimuombe askofu aongee na mzee, mimi nikamwambia siendi kokote, nikamwambia mama yule mzee ni hero (shujaa) hatobadilika, kweli sikwenda.”

“Nimekwenda kumtembelea gerezani mara nne, siku zote amebaki na msimamo wake licha ya magumu aliyopitia katika kipindi chote hicho, akasimamia kile alichoamini kuwa hajaiba na yuko tayari kutoa ushirikiano,” alisema Padri Massenge.

Paroko huyo alieleza kuwa kwa Rugemalira kuwa muumini wa parokia hiyo mengi yalizungumzwa baada ya kukamatwa, huku fedha zake zikihusishwa na ujenzi wa kanisa la Parokia ya Makongo Juu.

“Mambo mengi yalizungumzwa huko jimboni kuhusu Kanisa la Makongo, wapo waliosema tunakwenda kwa kasi kwa sababu ya hela za Escrow, nikawaambia kama mwenye ushahidi wa kwamba kuna senti imeingia hapa alete.

“Na leo nawapa siri, Mzee Rugemalira alinialika mara kadhaa niende nyumbani kwake lakini sikuwahi kupata nafasi, hivi ningekuwa nimeenda na kuna hela yoyote imeingia hapa kanisani, sijui tungekuwa na hali gani, ndio lingeitwa Kanisa la Escrow, lakini niwaambie haya yote ni mpango wa Mungu,” alisema.

Padri Massenge pia alimpongeza Rugemalira kwa uamuzi wa kwenda kanisani saa chache baada ya kuachiwa huru, huku akikumbushia siku aliyokamatwa.

Kauli ya Rugemalira

Uso wake ukionekana wa furaha na bashasha, Rugemalira aliupongeza uongozi wa kanisa kwa kufanisha ujenzi wa kisasa wa kanisa hilo ambao ulianza muda mfupi kabla ya kukamatwa kwake.

“Kiukweli niwapongeze kwa kazi kubwa iliyofanyika, kuwa na kanisa la aina hii yaani naona maajabu kila nikiangalia huku na kule,” alisema.

Pia mfanyabiashara huyo ambaye tangu awe mahabusu amekuwa na mwonekano wa tofauti wa kuacha nywele na ndevu nyingi, alitumia jukwaa hilo kueleza siri ya mwonekano huo.

“Juzi nilipokuja kumshukuru Mungu baada ya kuachiwa huru, nilimuomba baba paroko amwambie baby (mkewe) sininyoe hizi ndevu, maana alitaka kuninyoa.

“Nataka niwashuhudie kwamba hizi nywele na ndevu sijawahi kunyoa tangu niingie gerezani, nawashukuru kwa sala na maombezi yenu. Tuko pamoja,” alisema Rugemalira

Kauli hii ililifanya kanisa lilipuke kwa nderemo na vifijo kutoka kwa waumini ambao baada ya muda mfupi waliungana na wanandoa hao kutoa sadaka ya shukrani.

Hali ilivyokuwa

Rugemalira na mkewe waliwasili kanisani hapo saa 2:26 asubuhi kwa ajili ya misa ya pili na punde baada ya kushuka kwenye gari wakaanza kusalimiana na waumini wengine.

Baadhi ya waumini walisikika wakimpongeza Benedicta na kumkaribisha tena Rugemarila kanisani.

Baada ya kuingia ndani padre alimuita mbele Rugemalira awasilimie waumini naye aliitikia wito huo kwa kumtanguliza mkewe huku yeye akifuata nyuma.

Mara kadhaa wakati ibada ikiendelea Rugemalira alionekana akiangaza huku na kule kuliangalia kanisa hilo ambalo ujenzi wake umekamilika akiwa gerezani.

Misa ilipoisha alitoka nje akiwa ameambata na mkewe na kusalimiana na makundi ya waumini waliosogea karibu yao huku wakati wote akionekana kukunja mikono kwa ishara ya kushukuru.