Mkenda: Hakuna mtoto atakayekosa nafasi sekondari 2027
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na wakuu wa shule, walimu wakuu na maofisa elimu kata wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo wa uthibiti ubora wa shule kidigiti Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda amesema Serikali itatumia mbinu mbalimbali kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayeachwa mwaka 2027.
Rombo. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kila mwanafunzi atakayehitimu elimu ya msingi mwaka 2027 anaendelea na masomo ya sekondari bila vikwazo.
Akizungumza leo Julai 17, 2025 katika uzinduzi wa mafunzo ya mfumo wa kidijitali wa uthibiti ubora wa shule za msingi na sekondari wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro, Prof Mkenda amesema mwaka huo utakuwa wa kipekee kutokana na kuhitimu kwa wanafunzi wa madarasa mawili tofauti darasa la saba kwa mtaala wa zamani na darasa la sita kwa mtaala mpya.
“Tutatumia mikakati mbalimbali kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayebaki. Tunaweka akiba, tunajenga VETA kila wilaya, na hata baadhi ya VETA tunaweza kuzielekeza kutoa elimu ya sekondari kwa muda ili kupokea wanafunzi wote,” amesema Prof Mkenda.
Ameeleza kuwa Serikali pia itaingia makubaliano na shule binafsi za sekondari kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa Serikali kwa masharti nafuu ya ada.
“Tutaomba tutumie shule binafsi tuwalipie ada watoto wa Serikali endapo makubaliano yatakuwa mazuri. Hii itatusaidia kuhakikisha kila mtoto anaendelea na elimu,” amesema.
Prof Mkenda amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha angalau asilimia 75 ya wanafunzi wa darasa la saba na asilimia 100 ya wale wa darasa la sita wanajiunga na sekondari.
“Mwaka 2027 ni mwaka wa mageuzi makubwa ya elimu. Mahafali yatafanyika kwa madarasa mawili tofauti darasa la saba na darasa la sita, wote wakimaliza elimu ya msingi kwa pamoja,” amesema.
Katika kuhakikisha maandalizi yanaenda vizuri, Waziri huyo ameziagiza halmashauri zote nchini kuanza ujenzi wa madarasa ya sekondari katika maeneo ya shule za msingi zenye maeneo makubwa lakini zisizo na sekondari jirani.
“Tuna mpango wa kuhakikisha mtoto anaweza kutembea kwa mguu kwenda sekondari. Kwa hiyo, shule ya msingi yenye eneo kubwa ianze kujenga madarasa ya sekondari mwaka huu ili 2027 ianze kutumika,” amesema.
Kwa upande wake, Mthibiti Mkuu wa Ubora wa Shule wilayani Rombo, Mwalimu Abigael Mkama amesema mfumo wa kidijitali wa tathmini ya shule utasaidia katika ufanisi wa kazi na utoaji sahihi wa takwimu kwa wakati.
“Mfumo huu utatusaidia kupata taarifa kwa haraka na kwa usahihi ili wadau mbalimbali wa elimu waweze kuona maendeleo ya shule zote nchini,” amesema.