Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mlalamikaji kesi ya shambulio, awavunja mbavu watu kortini

Muktasari:

  • Adai kufanyiwa shambulio la kupigwa  na mwenzake, tukio lililofanyika  Januari 8, 2025 eneo la Upanga.

Dar es Salaam. Mkazi wa Upanga na raia wa India, Hussein Wangawaya (41), amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, kujibu shtaka moja la shambulio.

Wangawaya amefikishwa mahakamani hapo jana Ijumaa Januari 10, 2025 na kusomewa kesi ya jinai namba 7 ya mwaka 2025.

Mshtakiwa huyo amesomewa shtaka lake na karani wa Mahakama hiyo, Shabani Hamadi, mbele ya Hakimu Mkazi Scholastic Odoyo.

Karani Hamad amedai mshtakiwa ameshtakiwa chini ya kifungu 241 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Akimsomea shtaka lake, karani Hamad amedai kuwa mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo, Januari 8, 2025 saa 4:00 usiku eneo la Upanga.

Inadaiwa siku hiyo katika Mtaa wa Alikan uliopo wilaya ya Ilala, mshtakiwa kwa makusudi bila halali alimshambulia Jabir Patwa sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia maumivu.

Inadaiwa kuwa kitendo hicho ni kosa na kinyume cha sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mshtakiwa alikana shtaka lake na kuomba dhamana.

Hakimu Odoyo amesema dhamana ya mshtakiwa ipo wazi, hivyo anatakiwa awe na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh1milioni.

Mlalamikaji awavunja mbavu watu

Hakimu Odoyo baada ya kutoa masharti hayo, mlalamikaji katika kesi hiyo Jabir Patwa alisimama ghafla na kunyoosha kidole

Baada ya kusimama ndani ya chumba cha mahakama hiyo, alimuomba hakimu Odoyo, aweke masharti makubwa ya dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo, kwani kiasi alichoweka ni kidogo na sehemu ya maelezo yake ilikuwa kama ifuatavyo.

Jabiri: Mheshimiwa naona kiasi ulichoweka cha dhamana ni kidogo sana, nataka uongeze.

Hakimu: Unasema?

Jabiri: Hiyo pesa ya dhamana ya Husein ni ndogo sana.

Hakimu: Unataka tuweke shilingi ngapi?

Jabir: Naomba uweke zaidi ya milioni 10.

Hakimu: Kwa hiyo tuweke milioni 20?

Jabir: Ndio hapo utakuwa umenisaidia sana, maana aliniumiza sana huyu mshtakiwa.

Wakati Jabir akiomba Mahakama iweke masharti hayo, watu wote waliokuwepo awali walijizuia kucheka lakini baadaye walishindwa kuvumilia hali hiyo na hivyo kuangua kicheko kikubwa kilichomfanya hata hakimu naye acheke huku akimtizama kwa makini.

Hakimu Odoyo alimfafanulia mlalamikaji huyo kiasi hicho cha fedha ambacho mshtakiwa anatakiwa kusaini kupitia mdhamini wake ni dhamana kwa ajili ya kesi yake na sio faini wala fidia kwamba kesi hiyo bado inaendelea kwa tarehe ijayo.

Hata hivyo, pamoja na maombi hayo ya Jabir, Mahakama hiyo ilibaki na masharti iliyoyatoa awali ya mshtakiwa awe na mdhamini mmoja mwenye barua inayotambulika kisheria atakayesaini bondi ya Sh1milioni.

Mshtakiwa alifanikiwa kutimiza masharti hiyo na yupo nje kwa dhamana.

Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Januari 27, 2025.