Mlima Kilimanjaro waingizwa katika programu kubaini sababu za kupungua kwa barafu

Mlima Kilimanjaro uliopo Mkoa wa Kilimanjaro.
Muktasari:
- Uamuzi wa kuingizwa kwa Tanzania katika programu hiyo ulitangazwa wakati wa mkutano wa kamati Kuu ya Utendaji ya Shirika la Hali ya Hewa duniani uliofanyika mjini Geneva Uswisi
Dar es Salaam. Mlima Kilimanjaro uliopo Mkoa wa Kilimanjaro umejumuishwa katika programu ya kuboresha huduma za hali ya hewa kwa maeneo ya dunia yenye barafu ya asili.
Programu hiyo inayofahamika kitaalam kama Polar and High mountain regions itahusisha ufuatiliaji wa karibu kwa njia ya kupima utafiti ili kufahamu kwa kiwango gani barafu inapungua na sababu za kupungua.
Uamuzi wa kuingizwa kwa Tanzania katika programu hiyo ulitangazwa wakati wa mkutano wa kamati Kuu ya Utendaji ya Shirika la Hali ya Hewa duniani uliofanyika mjini Geneva Uswisi.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya hewa nchini, Dk Agnes Kijazi leo Juni 29, 2018 ameieleza MCL Digital kuwa mlima Kilimanjaro kuingizwa kwenye program hiyo kutazidi kuutangaza kimataifa hali itakayopelekea kuwavutia watalii wengi zaidi.
Sanjari na hilo amesema matokeo ya ufuatiliaji na utafiti yatasaidia kujipanga kwa namna ya kukabiliana na athari hizo zitakazobainika kusababisha barafu asilia kuyeyuka.
“Pamoja na kuwavutia watalii kuja kuona mlima Kilimanjaro matokeo ya ufuatiliaji huu yatatupa mwanga sasa tukabiliane vipi na athari hasa zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa ili kubadilisha hali inayoendelea sasa ya kuyeyuka kwa barafu hiyo,”amesema.
”Hii ni hatua kubwa zaidi kwa kuwa mlima huu ni wa kwanza katika ukanda wa tropiki wa Afrika hususan Afrika Mashariki na kati kuingizwa katika programu hii. Mlima Kilimanjaro ni mlima wa pekee na aina yake ulioko kwenye tropiki wenye barafu asilia,”