Mlinzi wa chuo akamatwa akituhumiwa kuiba gari

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi akionesha gari iliyokamatwa baada ya kuibiwa na mlinzi wa chuo kikuu cha Rucu.

Muktasari:

  • Inadaiwa kuwa mlinzi huyo wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (Rucu), aliondoka na gari hilo likiwa kwenye eeo la maegesho na alikutwa nalo wilayani Kilolo.

Iringa. Jeshi la Polisi Mkoani Iringa linamshikilia David Richard (23) Mlinzi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (Rucu) kwa tuhuma za wizi wa gari aina ya Toyota Raum mali ya Abraham Gasper (34) mfanyabiashara na mkazi wa Mkwawa.

Akizungumza na wanahabari mkoani hapo leo Alhamisi Desemba 8, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 30, 2022 mtuhumiwa aliiba gari hiyo ikiwa kwenye maegesho chuoni hapo.

“Mmiliki wa gari hiyo alipogundua wizi huo alitoa taarifa kituo cha polisi na msako kuendekea na hatimaye mtuhumiwa alipatikana Wilaya ya Kilolo akiwa na gari hiyo.

“Upelelezi umekamilika na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo,”amesema Bukumbi.

Katika tukio jingine, Kamanda Bukumbi ameeleza kuwa jeshi hilo limefanikiwa kumkamata Boni Kipalile mkulima mkazi wa Igangidungu anayetuhumiwa kujihusisha na matukio mbalimbali ya kihalifu.

Amesema mtuhumiwa huyo amekamatwa akiwa na silaha moja aina ya shortgun yenye namba 14949 ikiwa na risasi tatu moja ikiwa chemba.

“Baada ya kumkamata mtuhumiwa, alipekuliwa na kukutwa na pikipiki mbili moja yenye namba ya usajili MC19 CJV aina ya Boxer na nyingine haina usajili aina ya Kinglion Pamoja na spea za pikipiki,” amesema.

Aidha kwa kushirikiana na askari wa jeshi la uhifadhi, limefanikiwa kumkamata Benadetha Kipago (61) mkazi wa Izazi akiwa na jino moja la tembo la meno mawili ya mnyama kiboko.


Mbali na matukio hayo pia jeshi hilo limekamata watuhumiwa wawili wanojihusisha na matukio ya kihalifu ikiwemo wizi wa pikipiki ambapo katika nyakati na maeneo tofauti walikamatwa wakiwa na jumla ya pikipiki 9.

Bukumbi amesema kuwa katika tukio hilo mtuhumiwa Alfred Mkanula (25) fundi pikipiki alikamatwa akiwa na pikipiki 6 zote aina ya Sunlg na Emmanuel Mnyeke (28) alikamatwa na pikipiki 3 aina ya Boxer pamoja na vipuri vya pikipiki.