Mmoja afariki mafuriko Kilosa

Muktasari:

  • Mvua zinazoendelea kunyesha katika mikoa ya Manyara na Singida, zimesababisha kifo cha mtu mmoja (mwanaume) ambaye bado jina lake halijapatikana, wakati akijaribu kujiokoa baada ya maji kuingia katika nyumba yake.

Morogoro. Mtu mmoja  ambaye jina lake halijafahamika, amefariki wakati akijiokoa baada ya maji kuingia katika nyumba yake usiku wa kumkia leo, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku kucha eneo la Rudewa, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Desemba 5, 2023; Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amesema kifo cha mtu huyo (mwanamume) kimetokea baada ya yeye na mkewe, kujaribu kujiokoa, ndipo maji yalipomzidi na hivyo kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa DC Shaka, kifo cha mwanamume huyo kimetokea kati ya saa 11 na 12 asubuhi,  na mwili wake umepatikana.

"Kwa sasa kipaumbele ni kuwasaidia watu kutoka kwenye maji ili kusitokee madhara zaidi, baadhi ya nyumba zimebomoka kutokana na maji mengi ya mvua yalitokatiza kutoka katika mikoa ya Manyara na Singida.

“Maji hayo yamepasua kingo ndogo za mito ya Mkondoa na  Wami na kuleta madhara katika maeneo la Rudewa na Mvumi,”amesema.

Kwa upande wa mmoja wa wakazi wa Rudewa, Hamida Hamdan ameiambia Mwananchi Digital kuwa japokuwa mvua ilinyesha eneo hilo usiku kucha, lakini ilikuwa ya kawaida.

 “Kilichotushangaza ni kusikia mvumo wa maji yakipita kwa wingi, kabla hatujashtuka, maji yalianza kuingia kwenye nyumba za watu, tuliona nyumba zinaanguka maana eneo letu lote limejaa maji na watu wamekosa makazi kwa sasa,”amesema.


Taarifa zaidi zitawajia kupitia Mwananchi Digital.