Mnada wa Mnyagala hauna vyoo tangu umeanzishwa
Katavi. Wafanyabiashara wa mifugo zaidi ya 2000 katika mnada wa Mnyagala, wilayani Tanganyika, wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma ya vyoo tangu mnada huo uanzishwe 2012 ambapo inawalazimu kujisaidia vichakani jambo linalohatarisha afya zao.
Wakizungumza na mwananchi kwa nyakati tofauti kwa njia ya simu leo Agoust 31, 2023 baadhi ya wafanyabiashara wamesema licha ya kulipa ushuru bado halmashauri haijajenga vyoo katika eneo hilo.
Shigela Magembe mfanyabiashara wa ng’ombe amesema hali hiyo ni mbaya kiafya kwani wanaweza kupatwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na msongamano wa watu wanaofika mnadani hapo ikiwepo wale wanaotoka nchi jirani ya Kongo (DRC).
“Changamoto hii tumeiwasilisha mara kwa mara kwa viongozi akiwemo Diwani wa Kata ya Mnyagala lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea na mnada unafanyika mara mbili kwa mwezi Jumatatu na Jumanne,”
“Tunaiomba Serikali isikie kilio chetu, tunashangaa kwanini washindwe kujenga vyoo ilihali mapato wanakusanya? Mnada unakusanya watu wengi sana wafanyabiashara wa ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku na bidhaa zingine,” amesema Shigela.
Anna John, mfanyabiashara wa mgahawa, amesema kero hiyo inaweza kuhatarisha afya za jamii inayozunguka eneo hilo, kwani wanatumia maji ya visima walivyochimba kwenye makazi yao.
“Wakati wa masika hali ni tete maji ni mengi yanayotoka huko vichakani, mengine huingia katika visima tulivyochimba, na hatuna jinsi, inabidi tuyatumie, mamlaka husika ni kama hazioni, wao wanajali mapato pekee,” amesema Anna.
Katika kikao Baraza la Madiwani kilichoketi kwa ajili ya kupokea taarifa za kamati kwa mwaka wa fedha uliopita 2022/2023, Diwani wa Viti Maalum Kata ya Mnyagala, Amina Lumbwe, aliibua hoja hiyo akiungwa mkono na wengine
“Hali iliyopo Mnyagala ni mbaya, mwenyekiti niliomba angalau halmashauri iangalie uwezekano wa kujenga choo eneo la mnadani, halmashauri inachukua mapato pale huoni wanaweza kupata ugonjwa wa mlipuko?” amehoji Amina.
“Hili suala nimelipigia kelele mara kwa mara lakini cha ajabu halmashauri imekwenda kutekeleza eneo lako la Ikola, mimi niliomba ombi maalum kwanini hawajatekeleza?” amesema Amina.
Diwani wa kata hiyo, Mathias Nyanda, akagongelea msumari suala hilo kwa madai kuwa wasitishe kukusanya mapato hadi pale halmashauri itakapeleka mradi wa ujenzi wa vyoo.
“Wakikamilisha ndo waanze kukusanya mapato tofauti na hapo huo mnada ufungwe kwa sababu ni hatari kiafya, wananchi wanatuhoji tunakosa majibu,” amesema Nyanda.
Aidha Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Graison Mwanga amesema mnada huo unaiingizia mapato halmashauri sh600, 000 kila mwezi.
“Mnada unafanyika mara mbili kwa mwezi, kila siku ya mnada tunakusanya sh 300,000 ambapo kwa mwezi tunapata hizo Sh600, 000,”amesema Mwanga.
Kaimu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Philemon Mollo, akahitaji majibu ya kina kutoka ofisi ya Mkurugenzi, akihoji kwanini haijatatua changamoto hiyo.
“Hivi kweli halmashauri inakosa Sh2milioni za kujenga choo eneo hilo, toeni majibu ya kuwaridhisha madiwani na mtekeleze,” amesema Mollo.
Hatmaye Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Betuely Luhega, akaifunga hoja hiyo kwa madai kuwa watajenga choo cha dharura.
“Niwahakikishie kwamba haya ni maelekezo wala siyo ombi Mwenyekiti kaelekeza choo kijengwe mnada wa Mnyagala na sisi kama watekelezaji tumepokea tunakwenda kutekeleza,” amesema Luhega.