Mnyika awataka wananchi kuendeleza mapambano Katiba mpya

Katibu Mkuu wa Chadema,John Mnyika akizungmza katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika maeneo ya Manzese jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amewataka wananchi kuendeleza mapambano ya kupatikana katiba mpya itakayowapa nguvu ya kuiwajibisha Serikali.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amewataka wananchi kuendeleza mapambano ya kupatikana katiba mpya itakayowapa nguvu ya kuiwajibisha Serikali.

Mnyika ameyasema hayo leo Julai Mosi alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara eneo la Manzese jijini hapa, akisema, mbali na Katiba mpya chama chao pia kitaendelea kupigania upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi.

"Gharama za maisha zimeendelea kuwa juu, hiyo yote ni matokeo ya ubovu wa katiba mpya," amesema.

Mnyika amesema kamati kuu ya chama hicho itakutana kujadili masuala yanayowagusa wananchi ukiwamo mjadala wa mkataba wa uendeshaji na uboreshaji wa bandari kati ya Serikali ya Tanzania na Dudai.

Amewataka Watanzania kwa ujumla kuendelea kudai katiba mpya kwani jambo hilo ni ajenda ya msingi kwao.

Pia amegusia usafiri wa magari yaendayo haraka maarufu kama mwendo kasi, akishauri mabasi hayo kutumia gesi badala ya mafuta ili kupunguza gharama za nauli ya kusafiria kwa wananchi.

“Tuna kituo cha gesi ubungo kwa nini mabasi ya DART yasiwekewe mfumo wa gesi,” amesema.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Wananchi la chama hicho, Suzan Lyimo amesema wakati Tanzania ikielekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025 wananchi wanapaswa kuchagua viongozi sahihi kushika nafasi hizo.

Naye Mbunge wa viti maalumu Chadema, Bertha Mwakasege yeye amewataka wananchi waendelee kuleta kero zao ili serikali itambue changamoto wanazozipata na kukumbana nazo.