Moi yapokea vifaa tiba vya Sh3 bilioni

Muktasari:

  • Vifaa hivyo vitatumika katika upasuaji wa kubadilisha nyonga na magoti, urekebishaji wa misuli ya magoti kwa njia ya matundu, urekebishaji wa ulemavu kwa watoto na upasuaji wa tishu  pamoja na huduma nyingine za kibingwa.

Dar es Salaam. Jumuiya ya Mtakatifu Roch ya Uingereza imetoa vifaa tiba vya upasuaji katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MO), vyenye thamani ya Sh3 bilioni, vitasaidia uboreshwaji wa huduma za kibingwa kwenye taasisi hiyo.

Akipokea msaada huo leo Alhamisi Septemba 21, 2023; Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk John Jingu, amesema: “Msaada huu mkubwa...utasaidia kupunguza changamoto ya vifaa tiba na has kwenye upasuaji.”

Jingu amesema vifaa hivyo vitatumika katika upasuaji wa kubadilisha nyonga na magoti, urekebishaji wa misuli ya magoti kwa njia ya matundu, urekebishaji wa ulemavu kwa watoto na upasuaji wa tishu  pamoja na huduma nyingine za kibingwa.

Katika kuwajengea uwezo kwenye utoaji wa huduma za kibingwa, jumuiya hiyo, ikishirikiana na madkatari wa ndani, kwa pamoja watawahudmia wananchi wanaopata matibabu katika taasisi hiyo kwa muda wa siku nane.

Na katika hili, Dk Jingu amesema: “...itasaidia kukuza ujuzi kwa madaktari wachanga na pia italeta matokeo chanya katika utoaji tiba kwa wananchi...wageni wakiondoka haitakuwa Moi hii, kutakuwa na mabadiliko makubwa, hii ni fursa ya kila mmoja kujifunza, fursa hii itatoa matunda chanya na ya kudumu kwa jamii yetu.”

Mtendaji huyo wa Wizara ya Afya ameusifu ushirikiano huo huku akisema: “Ushirikiano huu unaenda kuimarika mahusiano baina ya Tanzania na Uingereza na matarajio yangu kwamba utakuwa endelevu na wenye tija kwa manufaa ya watanzania wote.”

Kwa upande wake, Kiongozi wa timu hiyo kutoka Uingereza, Dk Adil Ajuied, amesema lengo ni kubadilishana uzoefu na madaktari wa Moi katika tiba za mifupa, viungo, majeraha sugu na ajali.

Amesema kutokana na mapokezi waliopata wana imani ushirikiano huo utaendelea katika kujengeana uwezo wa kiujuzi kutokana na kukua kwa teknolojia za kitabibu.

“Nimetembea nchi nyingi, Afrika ya Kusini, Australia, India na Dubai lakini siajawahi kuona kiwango bora cha usafi kama hapa, watu wanawahi kuja na wanachelewa kuondoka, wanajituma na wanajivunia kuwa Moi,” amesema Dk Ajuied.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Profesa Abel Makubi, amesema ujio wa madaktari hao na utoaji wa msaada wa vifaa tiba, kutaleta matokeo chanya kwa MOI.

“Hii ni hospitali ya Taifa ya tiba ya mifupa, ubongo na ajali, tunatambua jitihada zetu katika kuasisi ushirikiano huu wa kudumu na hii itaongeza idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji kutoka 26 kwa siku hadi kufikia 42.

Makumbi amesema uwepo wa Madaktari hao kwa siku nane, una lengo la kusaidia utoaji wa matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa, na kwamba hospitali hiyo inakabiliwa na msongamano wa wagonjwa kutoka ndani na nje.