MOI yawapa mbinu majeruhi wa ajali

Kaimu Mkurugenzi wa MOI na daktari bingwa wa ubongo na mishipa ya fahamu, Laurent Lemery.

Muktasari:

  • Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imesema asilimia 94 ya majeruhi wanapokelewa kwenye taasisi hiyo wanafika kwa kuchelewa na kushindwa kufikia malengo ya kimataifa kuhakikisha mgonjwa wa ajali anatibiwa ndani ya saa moja tangu kutokea ajali 'saa la dhahabu.

Dar es Salaam. Asilimia 94 ya majeruhi wa mifupa na ubongo hupokelewa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) saa sita baada ya kutokea ajali kinyume na viwango vya kimataifa vinavyotaka wafikishwe saa moja ili kuokoa maisha yao.

 Ili kupambana na changamoto hiyo, MOI imetoa maelekezo kwa hospitali za rufaa Dar es Salaam na Pwani kuanza kurufani wagonjwa moja kwa moja kwa taasisi hiyo pasipo kupitia hospitali zingine ikiwemo Muhimbili ili kuokoa saa la dhahabu.

Hayo yamesemwa jana Agosti 18, 2023 katika kikao cha kimkakati baina ya MOI na hospitali za Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kwa lengo la kuboresha huduma kwa majeruhi wa mifupa,  mgongo na ubongo.

Katika kikao hicho kilichofanyika MOI kwa lengo la kuboresha matumizi ya ‘saa la dhahabu’ inayomtaka majeruhi kupata matibabu ya uhakika ndani ya saa moja tangu kutokea kwa ajali.

Mkuu wa kitengo cha utafiti MOI Dk Joel Bwemelo amesema kuchelewa kufikishwa majeruhi hospitalini hapo kunapunguza uwezekazo wa kunusuru maisha yao.

“Kuna saa moja la dhahabu linaloweza kuokoa maisha ya majeruhi tangu ajali itoke, hapa MOI asilimia 94 ya majeruhi huja masaa sita tangu kutokea kwa ajali, wakati huu ule muda wa saa la dhahabu la kuokoa maisha yake huwa limepita,"


Daktari bingwa wa mifupa Anthony Assey amesema miongoni mwa sababu za kucheleweshwa kwa majeruhi kufika MOI ni pamoja na utaratibu wa rufaa unaochokua muda mwingi na kwamba kikao hicho kinalenga kuboresha mfumo wa rufaa ili kuwawahisha wagonjwa kufika.

“Kitu cha msingi kabla ya kumrufani majeruhi, hakikisha umemuhudumia na amekuwa stahimilivu, tukumbuke kuna suala la barabara zetu, foleni, hivi vyote vinahitaji kuzingatiwa kwa kumuandaa majeruhi kuweza kuhimili hali hiyo ili asipate athari za pili," amesema Dk Assey.

Mratibu wa kikao kazi hicho Dk Bryson Mcharo amesema lengo ni kuondoa changamoto zinazozuia majeruhi kupatiwa matibabu ndani ya saa moja tangu kutokea kwa ajali.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Amana Dk Bryson Kiwelu ameipongeza MOI chini ya utaratibu mpya utakaowawezesha kumpa rufaa majeruhi kwenda MOI moja kwa moja bila ya kupitia hospitali zingine.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dk Laurent Lemery amesema kikao hicho kinalenga kutekeleza sera ya Wizara ya Afya ya kuboresha utoaji huduma na hasa kwa wagonjwa wanaopata rufaa kwa ajili ya kuja MOI kwa matibabu zaidi.