Mongella aagiza tani tano za saruji zilizoibwa hospitali ya Sekou Toure zirudishwe

Muktasari:
Mradi wa ujenzi wa jengo la mama na Mtoto lenye uwepo wa kuhudumia wagonjwa 261 kwa siku ulianza Oktoba 2017 huku ukitarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu.
Mwanza. Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella ametoa wiki moja kwa msimamizi wa mradi wa ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure, Moses Urio kurejesha mifuko 263 ya saruji iliyoibwa katika mradi huo.
Pia, amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Nyamagana, Juma Jumanne kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini wahusika wa wa tukio hilo ili hatua stahiki zichukuliwe.
Mongella amesema alipokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu wakikanusha kwamba walinzi wanaoshikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kuiba saruhi hiyo.
“Sitaji kuona uonevu na haiwezekani kila wizi ukitokea wanashikishwa watu ambao ni wa tabaka la chini hivyo nakuagiza OCD fanya uchunguzi hata kama aliyeiba ni Mkuu wa Mkoa akamatwe ili kama hawa walinzi hawahusiki waachiwe,” alisema Mongella
Mongella ameongeza kwamba; “Na wewe Kaimu Meneja wa TPA, ambaye ni msimamizi wa ujenzi wa jengo hili ninakupa wiki moja hiyo mifuko iliyoibwa irejeshwe,”
Ameeleza kutoridhishwa na kasi ya mkandarasi anayesimamia ujenzi wa Jengo hilo na kumtaka kukamilisha mradi huo ndani ya wakati.
Msimamizi wa mradi huo ambaye ni Kaimu Meneja wa TPA mkoa wa Mwanza, Moses Urio amsema saruji hiyo iliibwa Desemba 2020.
“Mabadiliko yaliyotokea kwenye mchoro wa jengo hili ndiyo yalisababisha tumeshindwa kwenda kwa kasi iliyotarajiwa ila tutajitahidi kufanya kazi usiku na mchana ili tuukamilishe kufikia Novemba mwaka huu maana mpaka sasa tuko asilimia 80,” alisema Urio.