Mourinho akandia wachezaji sare ya Arsenal

Muktasari:

Manchester imelazimisha sare katika mechi nne mfululizo na sasa iko juu kidogo ya timu zilizo hatarini kushuka daraja baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 nyumbani na Arsenal jana (Jumanne Desemba 5)


Manchester. Kocha Jose Mourinho amewatuhumu wachezaji wake wa Manchester United kuwa wanajipiga risasi miguuni baada ya kikosi kilichokosa baadhi ya nyota wake, kulazimisha sare ya mabao 2-2 na Arsenal jana usiku (Jumanne Desemba 5).

Matokeo hayo yameifanya Manchster kutoka sare katika mechi nne mfululizo.

United, iliyoanza mechi hiyo huku Paul Pogba na Romelu Lukaku wakiwa benchi, ilionyesha ari ya hali ya juu ya kusawazisha kila Arsenal walipotangulia kufunga; la kwanza likifungwa na Anthony Martial na baadaye Jesse Lingard kupata pointi moja.

Lakini, baada ya kufungwa na Manchester City na kutoka sare mbili dhidi ya Crystal Palace na Southampton, United sasa ina pointi 18 ikiwa nyuma ya vinara wa Ligi kuu ya England, Man City kwa tofauti ya pointi 18 na ikikaribia ukanda wa timu zilizo hatarini kushuka.

United pia iko chini ya Chelsea na Arsenal, ambayo haijapoteza mechi 20 mfululizo, kwa tofauti ya pointi nane katika v ita ya kuwania nne bora.

Na Mourinho, ambaye alishuhudia makosa ya David de Gea na Marcos Rojo, alisema timu yake inaendelea kujimaliza.

 

“Tulifunga mabao manne na kutoka sare ya 2-2. Hata katika mechi kama ya leo tuliyocheza vizuri, tulijipiga risasi miguuni," alisema kocha huyo Mreno.

"Wakati mwingine tunapoteza nafasi za wazi, wakati mwingine makosa ya mabeki, lakini leo kulikuwa na ari ya aina yake, mchezo mzuri.

“Tatizo letu ni kuweza kucheza kwa kiwango hiki bila ya makosa tuliyofanya na tulicheza vizuri sana na tulipofanya makosa tuliadhibiwa.”

Kuchanganyikiwa kwa Mourinho kunaeleweka kutokana na ukweli kwamba bao la kwanza la Arsenal lililofungwa katika dakika ya 26, lilitokana na makosa ya kipa David de Gea.

Chris Smalling aliikosa kona ya Lucas Torreira na kumpa nafasi Mustafi kupiga mpira kichwa bila ya kuzongwa, akiudundisha chini na baadaye kumponyoka kipa.

Bao la pili lilitokana na Ander Herrera kushindwa kuokoa vizuri mpira na kuusukumia wavuni wakati akiwa amezongwa na Lacazette.

Lakini United ilijibu mapigo dakika nne baadaye na kusawazisha kupitia kwa Herrera.

Kocha wa Arsenal, Unai Emery alisifu wachezaji wake kwamba walijituma zaidi baada ya kupoteza wenzao wawili walioumia.

“Najivunia wachezaji wangu na kipindi cha pili kilitufanya tujiamini. Tulitawala mchezo, Na kama kuna timu ilistahili ushindi, tulistahili zaidi," alisema Emery.

"Kwa sababu ya majeruhi wawili, kila mchezaji alijituma zaidi na kuwa na akili ya kutaka kupita vizuri kipindi kigumu na tuliweza kutawala mchezo kadri tulivyotaka."