Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpango wa shule salama kuhuisha maadili ya wanafunzi

Mkurugenzi wa Elimu na Utawala (DEA) Ofisi ya Rais - Tamisemi, Vincent Kayombo

Muktasari:

  • Serikali imewataka wadau wote wa mtoto nchini kuhakikisha usalama wa mtoto kuanzia nyumbani, shuleni na kwenye jamii ili kumsaidia mtoto huyo kukua kwenye makuzi mema na kupata elimu bora.

Dodoma. Serikali imesema kuwa ongezeko la vitendo vya ukatili kwa wanafunzi, linachangia mahali pa shule kuwa si sehemu salama.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Septemba 8, 2023 na Mkurugenzi wa  Usimamizi wa Elimu kutoka Tamisemi, Vincent Kayombo, kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo waratibu wa mpango wa shule salama na wasimamizi wa usalama wa jamii wa mikoa na halmashauri.

Kayombo amesema kupitia mradi wa shule salama, wanatarajia kuondoa changamoto za maadili kwa wanafunzi, zinazojitokeza kwa walimu, wazazi na walezi kukiuka sheria, kanuni na taratibu za malezi ya watoto na makuzi ikiwemo sheria ya ulinzi wa mtoto ya mwaka 2016.

Amesema endapo mpango huu utasimamiwa kikamilifu matunda yake yatasaidia kuwajenga wanafunzi kisaikolojia, kimakuzi kiakili na malezi ili kuongeza ufaulu wa kitaaluma.

Kayombo amesema mafunzo ya shule salama kwa wataalam yameonyesha changamoto za utekelezaji kwenye baadhi ya maeneo hivyo baada ya mafunzo hayo watawekeana mikakati ya namna bora ya usimamizi na utekelezaji wa shughuli za mradi huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Elimu kutoka Tamisemi, Hadija Mcheka amewataka Maofisa Ustawi wa Jamii na Mendeleo ya Jamii, kubaini viashiria vyote vinavyoonesha ukatili kwa watoto na kuchukua hatua za haraka.

Mcheka amesema suala la ukatili kwa watoto halionekani siku moja hivyo ni wajibu wao kuhakikisha kuwa watoto wanakuwa salama nyumbani, shuleni na katika jamii inayowazunguka.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi, Dk Charles Msonde, amesema suala la usimamizi na usalama wa mtoto ni la lazima kwani serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya elimu hivyo kama usalama hautakuwepo uwekezaji wote huo utakuwa ni bure.