Mradi wa Sh14 bilioni kuzinufaisha wilaya zinazohifadhi wakimbizi Kigoma

Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye.
Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limezindua mradi wa miaka minne wa kuimarisha mnyororo wa thamani wa kilimo cha wakulima wadogo (Kilimo Tija Kigoma), usawa wa kijinsia na amani katika wilaya tatu zinazohifadhi wakimbizi mkoani Kigoma.
Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh 14.7 bilioni unaofadhiliwa na watu na Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) na WFP umezilenga kambi za wakimbizi za wilaya za Kakonko, Kibondo na Kasulu.
Mwakilishi na mkurugenzi mkazi wa WFP, Sarah Gordon-Gibson, alisema mradi huo umejikita kwenye masuala ya kiuchumi, kijamii na kimazingira ya usalama wa chakula na lishe.
"Serikali ya Tanzania, KOICA na WFP zitashirikiana kuhakikisha usalama wa chakula na lishe kwa zaidi ya wakimbizi 200,000, kusaidia wakulima wadogo wa Tanzania, kujenga jamii zinazosaidia kupambana na mabadiliko ya tabianchi, na kukuza mshikamano wa kijamii na usawa wa kijinsia," alisema.
Mkurugenzi mkazi wa KOICA, alisema mradi unalenga kuisaidia Serikali kufikia asilimia sifuri ya njaa, pia unajikita kwenye usawa wa kijinsia na kudumisha amani na usalama katika wilaya hizo.
"Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia KOICA inasaidia kutimiza lengo hili kwa kuimarisha usalama wa chakula na lishe miongoni mwa watu walio katika mazingira magumu ili kuwapo na uhakika wa chakula na mahitaji ya lishe ya wakimbizi.
"Ili kufikia malengo KOICA itatoa dola 6,00,000 na WFP dola 420,000, mradi utawafikia wakulima wadogo elfu ishirini katika wilaya za Kakonko, Kasulu na Kibondo watakaonufaika moja kwa moja na wakimbizi 208,000 katika kambi za Nduta na Nyarugusu watanufaika pia kwa miaka miaka minne," alisema.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye aliishukuru WFP na KOICA kwa mradi huo huku akifafanua kwamba kitendo cha WFP kununua mazao moja kwa moja kutoka kwa AMCOS mkoani Kigoma ilikuwa ni moja ya mafanikio makubwa yaliyochangia kuimarisha uwezo wa wakulima wa mkoa huo na kuchangia uchumi wa ndani.
"Katika mradi huu tusiwaache wanawake na vijana nyuma, wao ndio injini muhimu ya ukuaji wa kijamii na kiuchumi, hivyo mradi uzingatie jinsi wanawake na vijana waweze kuwezeshwa ili waweze kuchangia maendeleo ya mkoa," alisema.
Mradi huo utasaidia wakulima wadogo katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara teule yakiwemo maharage, mihogo na mahindi, ambayo watayauza kwa wakimbizi, pia utasaidia katika kupunguza upotevu wa hifadhi baada ya mavuno kwa wakulima wadogo, na kutekeleza uhusiano wa amani kati ya jumuiya inayowakaribisha wakimbizi.