Msajili, Jeshi la Polisi mmebeba dhamana ya amani yetu

Muktasari:

  • Kwa muda mrefu kumekuwa na mvutano kati ya Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa, vyama vya siasa vyenyewe hasa vya upinzani na Jeshi la Polisi. Ukipekua Katiba ya nchi na sheria zetu unashindwa kuelewa kwa nini haya yanatokea.

Kwa muda mrefu kumekuwa na mvutano kati ya Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa, vyama vya siasa vyenyewe hasa vya upinzani na Jeshi la Polisi. Ukipekua Katiba ya nchi na sheria zetu unashindwa kuelewa kwa nini haya yanatokea.

Kama kila mdau wa siasa angeisoma kikamilifu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na sheria ya vyama vya siasa sura 258 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019, naamini tusingekuwa na mtanziko tulionao.

Leo hii Msajili wa vyama siasa ameitisha kikao cha kutafuta maridhiano kati ya vyama vya siasa na Jeshi la Polisi, ni jambo jema kukaa mezani lakini je, kama kila upande ungetimiza wajibu wake tungefika hapo?

Msajili amepanga Oktoba 21, 2021 kwamba ni siku wadau hao wangekutana, lakini vyama vya siasa vyenye ushawishi mkubwa vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na ACT-Wazalendo vimetangaza kutoshiriki kutokana na sababu mbalimbali.

Chadema, ambacho ndicho chama kikuu cha upinzani nchini na NCCR-Mageuzi vimeweka wazi msimamo wa kutohudhuria mkutano huo kwa kuwa mambo yanayolengwa kujadiliwa tayari yamewekewa msimamo na sheria.

ACT-Wazalendo na CUF wao wametoa sababu za kutoshiriki kikao hicho kwa sababu siku hiyo watakuwa wanahudhuria kongamano kubwa la kitaifa la kujadili amani ya nchi, lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Tangu mwanzo nimetangulia kusema kama kila mdau, hasa Msajili wa vyama vya Siasa na Jeshi letu la Polisi wangesimama kwenye sheria badala ya kufanyia kazi matamko ya kisiasa yasiyo na miguu ya kisheria ya kusimamia, tusingefika hapa.

Mathalan, Ibara ya 3(1) Katiba yetu ya 1977 imetamka nchi yetu ni ya kidemokrasia inayofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, lakini yanayoendelea nchini mwetu hayaakisi hata kidogo kama tuko chini ya mfumo wa kidemokrasia.

Ukisoma kifungu kile cha 11(1) (b) cha sheria ya vyama vya siasa, chama kinachotaka kufanya mkutano wa hadhara kinatoa notisi ili kupata ulinzi na vyombo vya usalama kwa lengo la kuhakikisha mkutano unafanyika kwa amani.

Sasa Msajili wa vyama vya siasa kama mlezi wa vyama vya siasa na msimamizi wa sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2019, alipoona Rais wa awamu ya tano na wa sasa wanazuia mikutano ya hadhara, hakuona ni uvunjifu wa sheria na Katiba?

Kwa sababu moja ya majukumu ya ofisi ya Msajili kulingana na kifungu cha 4(5) (a) cha sheria hiyo ni kusimamia sheria hii na kifungu kidogo (g) kinasema jukumu lingine ni kuishauri Serikali kuhusu masuala yanayohusu vyama vya siasa.

Lakini kwa karibu miaka mitano sasa, vyama vya upinzani vimezuiwa kufanya mikutano ya hadhara kwa tamko tu la kisiasa, Polisi wanazuia mikutano ya ndani ambayo haiko kwenye tamko la Rais lakini CCM, wanaendelea kama kawaida.

Katika makala zangu niliwahi kueleza kwa kirefu sana juu ya utawala wa sheria kwamba ndio suluhisho kwa sababu sheria ni kama msumeno, inakata mbele na nyuma, hivyo kama ni kuzuia mikutano tujiulize ni kwa sheria ipi?

Mwaka 1765 Lord Camden ambaye alikuwa Jaji Mkuu wa Uingereza aliwahi kusema hivi kuhusu watawala kufuata sheria: lf it is the law, it will be found in our books. If it is not to be found there, it is not law”.

Yaani kwa tafsiri yangu isiyo rasmi, Jaji anasema iwapo ni sheria, basi tutaiona kwenye vitabu vyetu vya sheria na iwapo haipo humo basi hiyo siyo sheria, sasa kwa msingi huo, Msajili anapokutana na wadau wanakwenda kujadili nini?

Kwa mtazamo wangu, Msajili atimize majukumu yake kama mlezi na jicho lake lisione mapungufu tu ya vyama vya upinzani na vilevile Jeshi letu la Polisi wawe waamuzi (referee) na waviache vyama vya siasa vishindane kwa sera, hoja na usawa.

Intelijensia ya Polisi isilenge tu mikutano ya vyama vya siasa vya upinzani wakati CCM inafanya mikutano ya aina hiyo hiyo lakini haizuiwi, ndio maana nasema Msajili na Jeshi letu la Polisi mna dhamana kubwa ya kusimamia amani yetu.

Yale yanayoruhusiwa na Katiba na Sheria zetu tuyaache yafanyike na anayevunja sheria ndio achukuliwe hatua na si kupiga ramli kuwa mkutano wa chama fulani cha upinzani utahatarisha amani, watu wanajiuliza kwa nini upinzani tu.


0656600900