Msajili, Zitto wavutana

Msajili, Zitto wavutana

Muktasari:

  • Wakati baadhi ya vyama vya siasa vikitangaza kutoshiriki mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutafuta maridhiano na wadau wengine, Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimesema kitakuwa na mkutano wa amani ambao kimemwalika Rais Samia Suluhu Hassan.


Dar es Salaam. Wakati baadhi ya vyama vya siasa vikitangaza kutoshiriki mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutafuta maridhiano na wadau wengine, Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kimesema kitakuwa na mkutano wa amani ambao kimemwalika Rais Samia Suluhu Hassan.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliitisha kikao cha vyama hivyo na Jeshi la Polisi alioupanga ufanyike Oktoba 21, lakini TCD mkutano wake utafanyika Oktoba 21 na 22.

Septemba 23, Jaji Mutungi alifanya kikao na uongozi wa Jeshi la Polisi jijini Dodoma na kusisitiza kuwapo kwa mkutano huo ambao Chadema pamoja na ACT Wazalendo vimetangaza kutoshiriki.

Jana, chama cha ACT Wazalendo kilitoa taarifa kutangaza kutoshiriki mkutano wa Msajili na Jeshi la Polisi na kikisisitiza kushiriki ule ulioitishwa na TCD.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma chama hicho, Salim Bimani ilisema walimwandikia barua Msajili kuwa kikao chake kimjumuishe Waziri wa Mambo ya Ndani.

“Hadi sasa hatujapata mrejesho wa suala hilo na mwelekeo ni kuwa kikao hicho kitakuwa cha Polisi na vyama vya siasa pekee,” imesema taarifa ya chama hicho kinachokosoa kauli ya mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro aliyoitoa kwenye kikao cha Msajili kuwa hakuna shida kuhusu mikutano ya nje bali tatizo lipo kwenye mikutano ya ndani ambayo sheria haisemi chochote kuihusu.

Bimani alisema mkutano huo wa TCD, utakaoanza Oktoba 21 hadi 22, utahudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan atakayefungua kabla ya kufungwa siku ya pili yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu Jaffar Haniu alipoulizwa kuhusu ushiriki wa Rais kwenye mkutano huo alisema: “Mpaka sasa hatufahamu lolote, kama atashiriki, tutatoa taarifa.”

Akizungumza kwa simu jana, Jaji Mutungi alisema hataki malumbano, kwani yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kuitisha kikao hicho.

“TCD wametangaza siku ya kufanya mkutano huo baada ya kusikia mimi nimeshapanga hivyo, kama waliona kuna hali hiyo walitakiwa waandike barua au kuja ofisini kuhusu utaratibu ulipangwa na kuona tunafanyaje,” alisema Jaji Mutungi.

Alisema alishaongeza na Zitto Kabwe ambaye ni Mwenyekiti wa TCD na aliandika barua ya kuvialika, hata hivyo hakuwa na uhakika na vyama vilivyothibitisha kushiriki mkutano huo.

“Wasipohudhuria sawa kwa sababu sio mara ya kwanza kusema hivyo. Vyama viko 19 hata vikikataa vyama vitatu kwa sababu zao zingine,” alisema Mutungi.

Kwa upande wake, jana, Zitto amemwandikia barua Msajili akimtaka kutafakari upya siku aliyoitisha mkutano na vyama vya siasa na Polisi ili kuondoa mgongano wa tarehe.

“Tumewaalika viongozi wa dini, wadau wa maendeleo, na taasisi zisizo za kiserikali, kwa hiyo mkutano wa TCD ni muhimu zaidi na vyama wanachama wanaupa kipaumbele,” alisema Zitto.

Alisema vyama vingine kama Chadema, NCCR-Mageuzi vilishatangaza kutoshiriki mkutano wa Msajili huku CUF wakimuomba Msajili kuusogeza mbele wakati CCM haiathiriki na ukiukwaji wa sheria na utaratibu unaofanywa na Jeshi la Polisi kwa vyama vya siasa.

Jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Bara, Benson Kigaila alisisitiza kuwa chama chake hakitoshiriki kwenye mkutano huo ulioitishwa na Msajili.

“Msimamo wetu wa mwanzo bado haujabadilika, tulishasema kuwa hatutoshiriki mkutano huo lakini mambo mengine siwezi kuzungumza zaidi tunabakia hivyo,” alisema.

Naye Mkuu wa Idara ya Uenezi na Uhusiano wa Umma wa NCCR Mageuzi, Edward Simbeye alitoa msimamo kama huo kwa kuwa waziri hatokuwapo.