IGP: Sheria haielezi nini maana ya mikutano ya ndani

Muktasari:

  • Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro amesema kuna changamoto ya kutokuwepo sheria inayoeleza maana ya mikutano ya ndani.

Dodoma.  Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro amesema kuna changamoto ya kutokuwepo sheria inayoeleza maana ya mikutano ya ndani.

Ameyasema hayo leo Alhamisi Septemba 23, 2021 alipokutana na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mikutano ya vyama vya siasa na changamoto zinazojitokeza baina ya jeshi hilo na baadhi ya vyama.

“Jambo la kwanza tulikuwa tunaangalia changamoto zinazojitokeza kwa baadhi ya vyama vya siasa ambavyo vimekuwa vikilalamika kuzuiwa kufanya mikutano yao ya ndani” amesema Sirro.

Jaji Mutungi: Kumbe wakati mwingine Polisi wana nia njema

Naye Jaji Mutungi amesema kupitia kikao hicho yapo mambo waliyoyachukua ambayo watayaunganisha na mengine watakayoyapata kwenye kikao na vyama vya siasa.

"Hata hawa wanasiasa tutawaeleza mambo yaliyosemwa na wadau wengine ikiwemo Jeshi la Polisi. Msingi wa vikao hivi ni kutaka kupunguza misuguano isiyokuwa ya lazima na leo nimegundua wakati mwingine polisi wanakuwa na nia njema lakini raia tumekuwa hatujui,” amesema Jaji Mutungi.