Mshtakiwa adai kutibu Ukimwi kwa kutumia kobe, ngozi ya nyati

Mshtakiwa Matimba Washa

Muktasari:

  • Mkazi wa Kijiji cha Nyarukoru, mkoani Mara, Matimba Washa (28), ameshitakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Butiama kwa makosa matatu likiwamo la kukutwa na kobe 998, magamba 10 ya kobe, ngozi ya Nyati na mkia wa Nyumbu, vyote vikiwa na thaman ya Sh168 milioni.



Butiama. Mkazi wa Kijiji cha Nyarukoru, mkoani Mara, Matimba Washa (28), ameshitakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Butiama kwa makosa matatu likiwamo la kukutwa na kobe 998, magamba 10 ya kobe, ngozi ya Nyati na mkia wa Nyumbu, vyote vikiwa na thaman ya Sh168 milioni.

Mshtakiwa huyo akidai ameoteshwa na mapepo kuwa nyara hizo za Serikali ni tiba ya magonjwa kama vile ukimwi, seli mundu na magonjwa ya zinaa.

Washa aliwaambia Polisi katika mahojiano kuwa dawa yake ina uwezo wa kutibu magonjwa hayo. Pia alitoa maelezo hayo mahakamani na kuwaomba washitaki wake wamletee mahakamani hapo mtu   yeyote mwenye ugonjwa mmojawapo ili awathibitishie uwezo wa dawa hizo.

Kijana huyo amefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Julieth Semkiwa, leo Alhamisi Februari 2 2023.

Mwendesha mashtaka, wakili wa serikali Gaston Kayombo amesema mshtakiwa huyo anashtakiwa kwa makosa matatu ya kukutwa na nyara za serikali pamoja na uhujumu uchumi.

"Mashtaka haya yapo mahakamani hapa chini ya kifungu cha 86 kifungu kidogo cha 1 na cha 2(c), 3(c) ya Sheria ya Wanyamapori, Sura ya 283 marejeo ya 2022 ikisomwa na aya ya 14 ya jedwali la kwanza la kifungu cha 57 na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumilk, Sura ya 200 ya mwaka 2022" amesema Kayombo

Amesema kwa mara ya kwanza mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Januari 11 mwaka huu baada ya kukamatwa na nyara hizo.

Yafuatayo ni mazungumzo kati ya hakimu na mshtakiwa huyo mahakamani.

Hakimu: Matimba unaendeleaje?

Mshtakiwa:  Kiafya niko sawa ila kimawazo sipo sawa

Hakimu: Kwanini haupo sawa

Mshtakiwa: Mahali nilipo sio sahihi nataka kurudi nyumbani

Hakimu:  Kwahiyo bado unasisitiza kuwa aletwe mtu umfanyie tiba ili tuone kama dawa zinafanya kazi?

Mshtakiwa: Ndiyo

Hakimu: Unavyo vitendea kazi?

Mshtakiwa: Hapana hapa sina

Hakimu: Sasa utafanyaje wakati hauna vitendea kazi

Mshtakiwa:  Nchi hii ina viongozi kila sehemu kwahiyo vitu vinaweza kufuatwa na tukafanya majaribio

Hakimu:  Sawa utarudi hapa tarehe 16 kesi hii itakapotajwa, upelelezi bado unaendelea.