Mshtakiwa kesi ya kina Sabaya akana kuvamia duka

Mshtakiwa kesi ya kina Sabaya akana kuvamia duka

Muktasari:

  • Sylvester Nyegu (27),  mshtakiwa wa pili katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya amekana kuwepo katika  duka la Shahidi Store linalodaiwa kuvamiwa Februari 9, 2021.


  

Arusha. Sylvester Nyegu (27),  mshtakiwa wa pili katika kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya amekana kuwepo katika  duka la Shahidi Store linalodaiwa kuvamiwa Februari 9, 2021.

Nyegu ameeleza hayo leo Ijumaa Agosti 20, 2021 wakati akitoka ushahidi wake mbele ya hakimu mkazi mwandamizi,  Odira Amworo akibainisha kuwa  siku ya tukio hilo hakuwa Arusha.

Sehemu ya mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo;

Wakili: Shahidi hebu iambie mahakama 9/2/2021 majira ya saa 12 jioni hadi saa nne usiku ulikuwa wapi?

Shahidi: Nilikuwa nyumbani Bomang'ombe

Wakili: Bomangombe ni Wilaya gani na Mkoa Gani?

Shahidi:Ni mamlaka ya mji mdogo iliyopo Wilaya ya Hai, mkoa wa Kilimanjaro

Wakili: Sasa shahidi kuna mashahidi wamekuja katika mahakama hii wakatoa ushahidi 9/2/2021 wewe ulikuwa Arusha dukani kwa Mohamed Saad Hajirin una nini cha kuiambia Mahakama?

Shahidi: Ni uongo kwa sababu sifahamu kitu hicho,sipafahamu hapo ambapo mashahidi walipataja

Wakili: Hapa mahakamani unashitakiwa na makosa matatu ya unyanganyi wa kutumia silaha unaiambia nini mahakama?

Shahidi: Hayo ni mashtaka ya uongo, siyafahamu na hakuna shahidi yoyote aliyeletwa hapa mahakamani aliyesema kwamba nimefanya kitu chochote kuhusiana na mashitaka hayo kwamba nimeiba Sh2.769, milioni kwamba nimempiga mtu yoyote kati yao, kwamba nimemfunga pingu, kwamba nimeiba Sh390,000 na kwamba nimeiba Sh35,000 na simu ya Tecno Pop 1, hakuna shahidi aliyesema hayo.


Wakili: Shahidi unasema mashtaka ni ya uongo lakini kuna shahidi namba mbili, nne na sita walisema wamekuona dukani hapo una nini cha kuiambia mahakama?

Shahidi: Ushahidi wao ni wa uongo,uliojichanganya

Wakili:Hebu ikumbushe mahakama shahidii wa pili Numan Jasin alisema amekutambuaje?

Shahidi: Shahidi huyo alisema alinitambua sura nilipokuwa nyumbani kwao namkabidhi simu,ndipo alipotambua sura yangu lakini hakuweza kunitambua sura hapo dukani alipodai na kulikuwa na mwanga mkali

Wakili: Hebu iambie mahakama ni wakati gani shahidi aliweza kutambua jina lako

Shahidi: Kwenye maelezo yake niliyosikia hapa mahakamani hakuweza kuyatambua majina yangu

Wakili: Hebu iambie mahakama shahidi wa nne alisema amekutambuaje?

Shahidi: Shahidi namba nne alisema alitambua sura yangu nilipokuwa kwenye duka lakini hakuweza kutambua majina yangu

Wakili:Hebu iambie mahakama shahidi wa sita alisema alikutambuaje wewe?

Shahidi: Shahidi huyo alisema alinitambua kwenye moja ya gari ambapo alidai niliendelea kubaki kwenye hilo gari na sikushuka popote na sikuongea chochote

Wakili: Shahidi hebu ikumbushe mahakama kulingana na shahidi wa sita anasemaje kuhusu mlipita njia gani kutoka dukani kufika polisi?

Shahidi: Shahidi huyo amesema gari hilo ambalo na mimi nilikuwepo halikupita pengine popote hadi tulipofika polisi

Wakili: Hebu fafanua

Shahidi: Anapingana na shahidi mwenzake wa pili anayedai aliniona nyumbani kwao

Wakili: Shahidi,umesema shahidi wa pili,nne na sita walikutambua kwa sura lakini hawakujua jina lako ni lini gwaride la utambuzi lilifanyika wakakutambua?

Shahidi:Sikuwahi kufanyiwa gwaride lolote la polisi la utambuzi

Wakili: Shahidi umesema mashahidi hao walikutambua sura lakini hawakukufahamu jina lakini wamekuja mahakamani wakasema wewe ndiye Sylvester wakakugusa hilo linawezekanaje

Shahidi: Linawezekana kwa sababu tangu nimeletwa hapa mahakamani jina langu limekuwa likitamkwa na kutangazwa kwenye vyombo vya habari

Wakili: Vipi kuhusu sura yako

Shahidi: Picha zimekuwa zikisambaa kwenye hivyo hivyo vyombo vya habari na hata kuna shahidi wao alikuja na kudai kwamba aliniona kwenye TV nikiwa naletwa mahakamani(shahidi wa saba)

Wakili: Shahidi wa jamhuri namba sita alisema 9/2/2021,wewe ndiye ulichukua mfuko uliokuwa kaunta uliokuwa na fedha,nyaraka na mashine za EFD's,una kitu gani cha kuiambia mahakama kuhusu hilo?

Shahidi: Shahidi huyo ni muongo kwa sababu hapo alipopasema sipafahamu na pia sina hilo shtaka la kuchukua hizo EFD hapa mahakamani na kama ingekuwa kweli ningekuwa na shtaka hilo maana pia ni mali zao.