Msigwa ataka usawa wa jinsia kwa wanahabari

Msemaji mkuu wa Serikali Gerson Msigwa.
Muktasari:
- Msemaji mkuu wa Serikali Gerson Msigwa ametoa wito kwa vyombo vya habari nchini kuhakikisha wanaweka sera zinazosimamia masuala ya kijinsia ili kuwapo usawa unaoonekana kupotea huku wanawake wakiathirika zaidi.
Dar es Salaam. Msemaji mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amevitaka vyombo vya habari nchini kuwa na sera zinazosimamia masuala ya kijinsia, ili kujiepusha na unyanyasaji wa kijinsia unaoathiri Zaidi wanawake.
Msigwa ameyasema hayo leo Januari 21, 2023 katika uzinduzi wa tawi la taasisi ya Wanawake katika Habari (Women in News Tanzania Alumnae chapter) jijini hapa, akihamasisha uwezeshwaji wa wanawake katika tasinia ya habari.
"Vyombo vyote vya habari vinatakiwa kuwa na sera itakayo simamia masuala ya unyanyasaji wa kijinsia, ili kukomesha vitendo visivyofaa, ambapo wanawake wengi wanaoneka ndio waathiriwa wakuu na jambo hili litasimamiwa na idara ya Habari Maelezo," amesema
Msigwa amesema unyanyasaji wa kijinsia umewakosesha wanawake wengi fursa za kufanya kazi, hivyo amesema atasimama imara kuhakikisha unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake katika vyumba vya habari unakwisha.
"Mimi nipo tayari kukabiliana na wale wanaofanya unyanyasaji wa kijinsia dhidi yenu, hivyo msikate tamaa, najua changamoto ni nyingi ila zitatamatika," amesema
Pia amewaasa wanawake kuendelea kuhakikisha wanaifanya kazi yao kwa ufasaha bila kurudi nyuma kwa kuwa wapo wanao waangazia wao kama kioo.
"Napenda kuwaambia msikate tamaa kwani mnapo kata tamaa, mtakuwa mnawakatisha tamaa wale wanaotaka kuwa nyie kujiunga na vyombo vya habari," amesema.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Dk Joyce Bazira amesema utafiti uliofanywa na WIN kuhusu unyanyasaji wa kijinsia wanaopitia wanawake katika vyumba vya habari unaonesha mwanamke mmoja kati ya wawili hufanyiwa unyanyasaji wa kingono.
"Nchini Tanzania asilimia 47 ya wanawake wamefanyiwa unyanyasaji wa maneno huku asilimia 38 wamepitia unyanyasaji wa kingono wa kimwili ambapo kati ya hao asilimia 21 tu, ndio walioripoti adha hiyo," amesema.
Dk Bazira pia amesema wanawake wanatakiwa kusema yale wanayopitia wakiwa katika sehemu za kazi sio kukaa kimya, kwani kwa kufanya hivyo kutawasidia kutatua changamoto wanazopitia.
Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa WIN, Jane Godia amesema anaishukuru serikali kwa kuruhusu uhuru wa vyombo vya habari, jambo ambalo ni jema katika jamii za sasa, kwa kuwa kila jamii inayao haki ya kutambua kile kinacho endelea duniani.