Mtaala mpya kuwanoa wauguzi mbioni

Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi wa Ubora wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya,  Saturini Manangwa

Muktasari:

  • Mwaka 2022 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ilizitaja sehemu za kutolea huduma za afya kuwa miongoni mwa mamlaka tano za juu zinazolalamikiwa na wananchi kutokana na utoaji mbovu wa huduma nchini

Dodoma. Ili kukabiliana na malalamiko ya wananchi kuhusu huduma mbovu zinazotolewa na baadhi ya wauguzi, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Hawze na Umoja wa Ulaya (AU) imedhamiria kutengeneza mtaala mpya utakaofundisha namna ya utoaji bora wa huduma kwa wauguzi.

Mwaka 2022 Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ilizitaja sehemu za kutolea huduma za afya kuwa miongoni mwa mamlaka tano za juu zinazolalamikiwa na wananchi kutokana na utoaji mbovu wa huduma nchini.

Kutokana na matukio hayo ya ukosefu wa maadili kazini Baraza la Uuguzi na Ukunga liliwafikisha Mahakamani watu nane na kuwafutia usajili wauguzi 12 waliokutwa na hatia ya makosa ya kimaadili.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi msaidizi wa usimamizi wa ubora wa huduma za uuguzi na ukunga Wizara ya Afya, Saturini Manangwa amesema mradi huo wa miaka mitatu umelenga kuimarisha utoaji mafunzo ya huduma bora kwa wauguzi na wasimamizi wa hospitali.

“Tunakwenda kuimarisha mfumo wa utoaji huduma ambao unamjali mteja, ile huduma ambayo inapatikana kwenye hoteli na mashirika ya biashara tunaangalia ni kwa namna gani tunaenda kuiweka kwenye huduma za Afya.

Kwa kuanzia tumeanza na vyuo vikuu na tuna mpango wa kuvifikia vyuo vya kati kupitia mtandao” amesema

Manangwa amesema lengo la mradi huo ni kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi na kuhakikisha matakwa yao yanasikilizwa kwenye huduma kwani mitaala hiyo itazingatia mafunzo ya kutoa huduma zenye staha, kujali na utu.

Amesema kupitia mradi huo wakufunzi wa vyuo vikuu takriban 30, wakufunzi kwa vitendo wanaopatikana hospitali 35 na wanafunzi wa mwaka wa masomo uliopita takriban 150 katika vyuo vikuu vya afya vya Muhimbili, KCMC na Bugando.

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Hawze, Joya Smit amesema mradi huo umelenga kutoa elimu kwa watoa huduma ili kufanikisha utoaji bora wa huduma katika maeneo ya kutolea huduma za afya nchini.

Naye Mkuu wa shule ya uuguzi Chuo kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Dk Dickson Mkoka ambaye amepata mafunzo hayo amesema tangu mwaka 2021 walianza kutengeneza mtaala ambao unalenga kutengeza wanafunzi katika kutoa huduma za staha, kujali na zenye utu.

“Mahitaji katika soko la afya ni wananchi kupata huduma bora na sasa kipimo kimojawapo cha huduma ni pale ambapo muuguzi ana uwezo wa kutoa huduma zinazoweza kujali heshima, kuzingatia upendo na kutunza maadili, na suala hili kwa muda mrefu limekuwa ni changamoto” amesema