Mtaka awaagiza viongozi Ludewa kuhamasisha uwekezaji mazao ya biashara
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka (wa kwanza kushoto) akiwa kwenye kikao na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa.
Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka amewaagiza viongozi wa Wilaya ya Ludewa kuwahamasisha wananchi kuwekeza kwenye mazao ya biashara ili yawasaidie uzeeni.
Ludewa. Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka amewaagiza viongozi wa Wilaya ya Ludewa kuwahamasisha wananchi kuwekeza kwenye mazao ya biashara ili yawasaidie uzeeni.
Agizo hilo alilitoa jana Jumamosi Agosti 27, 2022 alipofanya ziara wilayani humo kuhamasisha Sensa ya Watu na Makazi ambayo ilianza Jumanne Agosti 23 mwaka huu.
Amesema anataka kuona wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) waliopo sasa wawe kizazi cha mwisho na pasiwepo wengine kwa kuwa fursa za kiuchumi zilizopo wilayani humo ni nyingi.
“Ni vizuri tuseme kwamba tutafika kizazi cha mwisho pengine hawa masikini wa Tasaf waliopo leo tuseme wazi kitakuwa cha mwisho kwa kuwa tunazo fursa nyingi za uchumi zinazoweza kututoa huko "amesema Mtaka.
Amesema anataka kuona kizazi kilichopo sasa kwanza kinakuwa na elimu ambayo itakuwa mkombozi kwa upande wao na kuleta mtazamo tofauti utakaolisaidia Taifa hapo baadaye.
Amemwagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa kuanza kuweka rekodi ya vijana wanaofanya vituko mitaani kwa kuzingatia wasifu wao ili rekodi hiyo ije kutumika uzeeni watakapo kwenda kuomba kuingizwa kwenye Tasaf.
“Tunataka tuanze kuweka rekodi za vijana wote wanaofanya vituko sasa kwenye ujana wao ili tuje tuitumiq uzeeni mtu akiuza shamba lake au la baba yake tunaweka kwenye rekodi, mtu akigoma shule tunaweka kwenye rekodi, mtu akifukuzwa kazi kwasababu ya ulevi naye tunamuweka kwenye rekodi ili akizeeka masikini na akahitaji msaada wa Tasaf tunamwonyesha vituko alivyofanya ujanani.” amesema Mtaka
Amewataka wazazi wilayani humo kuhakikisha wanawasomesha watoto wao ili wapate ujuzi ambao utawasaidia kujiajiri na kuajiriwa kwenye kampuni mbalimbali.
Amesema Ludewa ni wilaya ya kimkakati yenye miradi mikubwa ya Liganga na Mchuchuma ambayo hivi karibuni itaanza utekelezaji wake hivyo watoto wao wasije kuwa vibarua au kukosa kabisa ajira kutokana na kukosa vigezo vya kielimu.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Andrea Tsere amesema wanaendelea na shughuli za uhamasishaji uwekezaji kwa wananchi kwa kurejesha baadhi ya mazao yaliyokuwa hayapewi kipaombele.
“Ludewa pana ardhi nzuri kwa kilimo, mazao mengi ya biashara yanakubali hapa sasa tupo tunafanya uhamasishaji wa kilimo cha mazao ya biashara na kurejesha baadhi ya mazao yaliyo sahaulika mfano korosho kwa sasa hapa Ludewa kwa mwaka tunavuna tani 150, lakini pia tumeleta zao la parachichi awali huku walikuwa wanalima miti ya mbao tuu.” amesema Tsere
Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga amesema Serikali imetenga Sh16 bilioni kwa ajili ya ulipaji wa fidia kwa watu waliopisha maeneo yao kutokana na mradi wa Mchuchuma na Liganga.
Amewataka wananchi kufanya uwekezaji kwenye nyanja zote za kiuchumi ili miradi hiyo itakapofunguliwa wawe na njia nyingi za kujiongezea kipato na kujikimu kimaisha.