Mtandao wa kijamii Jeshi la Polisi wadukuliwa, latangaza msako mkali

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Tanzania limeonya na kutangaza msako waliosambaza taarifa za uongo, upotoshaji na zisizo na maadili kwenye mtandao wa kijamii wa jeshi hilo.
Limesema taarifa hizo zina lengo la kutaka kuuaminisha umma kuwa zimetolewa na Jeshi la Polisi kupitia mtandao wake wa X (zamani Twitter).
Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo leo Jumanne, Mei 20, 2025 imesema taarifa zinazosambazwa siyo za kweli likisisitiza Jeshi la Polisi haliwezi kuandaa na kusambaza taarifa kama hizo katika mitandao yake ya kijamii.
"Wakati tunaendelea kufuatilia wahalifu waliotengeneza na kusambaza taarifa hizo ili wakamatwe, tunawaomba wananchi wazipuuze taarifa hizo na kuepuka kuendelea kuzisambaza endapo zitakufikia," imesema taarifa ya jeshi la polisi.
Imesisitiza hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote yule aliyehusika na utengenezaji na utoaji wa taarifa hizo na yule atakayeendelea kuisambaza.
Taarifa ya Polisi imetolewa baada ya tukio la usiku wa kuamkia leo Jumanne, watu wasiofahamika kuingia katika akaunti ya kijamii ya Polisi na kuanza kuchapisha taarifa mbalimbali ambazo Polisi imefafanua kuwa haihusiki nazo na kuanza kuwasaka waliohusika