Mtangazaji Fredwaa afariki ajalini

Saturday June 12 2021
Fredwaa pc
By Aurea Simtowe

Dar es Salaam. Mwandishi wa habari Fred Fidelis maarufu Fredwaa amefariki  katika ajali ya gari iliyotokea leo Jumamosi Juni 12, 2021 saa 8 mchana Kawe mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Kamanda wa Polisi mkoa wa kipolisi Kinondoni, Ramadhani Kingai amesema chanzo cha ajali hiyo ni ulevi na kwamba wanamshikilia dereva wa gari hilo.

“Inaonekana dereva alikuwa amelewa wakati akiendesha gari liliacha njia na kuingia mtaroni eneo la Tanganyika Packers karibu na sehemu ambayo Mchungaji Boniphace Mwamposa huwa anatoa neno, mtangazaji (Fredwaa) alifariki ila dereva tunamshikilia,” amesema Kingai.

Amesema kwa mujibu wa taarifa hata Fredwaa hakuumia ila inaonekana alipata mshituko kwani dereva hajaumia.

Fredwaa amewahi kufanya kazi Times FM Dar es salaam, Radio Free Africa Mwanza pamoja na Clouds FM Dar es Salaam.

Advertisement