Prime
Mtanzania aliyetekwa Nigeria aachiwa, baba mzazi afunguka
Dar es Salaam. Siku moja baada ya kuachiwa huru Melkiori Mahinini (27), Mtanzania aliyetekwa nyara nchini Nigeria, baba yake, Dominic Mahinini amesema taarifa hizo zimemfurahisha na kiu yake ni kuonana naye kabla hajaendelea na shughuli zake.
Melkiori alitekwa Agosti 3, mwaka huu nchini humo alikokwenda kuishi mwaka mmoja wa kichungaji kabla ya kuanza masomo ya Teolojia, akiwa na raia wa Mali, Padri Paul Sanogo.
Wawili hao waliachiwa huru usiku wa kuamkia jana wakiwa salama baada ya kushikiliwa kwa siku 20 na watekaji waliotaka kupewa Naira 100 milioni (zaidi ya Sh170 milioni) ili wawaachie huru.
Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu kuachiwa kwa Melkiori, Mahinini, anayeishi mkoani Kigoma alisema alipata taarifa hizo kwa mara ya kwanza kutoka kwa mwandishi wa habari alipompigia simu.
Alisema angependa mtoto wake arudi kwanza nyumbani ili amuone, baada ya hapo aendelee na shughuli zake huko Nigeria. Alitoa shukrani zake kwa Serikali kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria na Kanisa Katoliki kwa msaada wao uliofanikisha jambo hilo.
“Ningependa aendelee na shughuli zake huko Nigeria kama Mungu alivyompangia, lakini aje kwanza nimuone,” alisema Mahinini wakati akizungumza kwa njia ya simu akiwa Kigoma.
Aliwashukuru Watanzania kwa kumwombea kijana wake hadi amepatikana na aliwaomba waendelee kumwombea ili atimize malengo yake.
Kwa upande wake, Katibu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Padri Achiles Charukula alisema wanamshukuru Mungu pamoja na waumini wote waliokuwa wakimwombea na sasa maombi yao yametimia.
“Tunaishukuru Serikali ambayo kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria wameshiriki kutusaidia. Tunatoa shukrani pia kwa gazeti la Mwananchi, walikuwa wa kwanza kupeleka habari hii, taarifa zikaifikia Serikali wakachukua hatua,” alisema Padri Charukula.
Padri Charukula, ambaye pia ni Katibu wa Askofu wa jimbo la Kigoma, aliishukuru pia Serikali ya Nigeria, jimbo la Niger na shirika la Wamisionari wa Afrika kwa ushirikiano walioutoa kwao.
Akizungumzia kuachiwa huru kwa Mtanzania huyo, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dk Benson Bana aliwashukuru Watanzania kwa maombi yao yaliyowezesha kuwa huru kwa kijana huyo.
Alisema njia zote zilitumika kuhakikisha kwamba kijana huyo na mwenzake wanapatikana wakiwa hai na wamefanikiwa kuwaokoa vijana hao wakiwa salama na sasa wanafanyiwa uchunguzi wa afya zao.
“Wote wako salama, wamedhoofika tu lakini ni wazima. Melkiori anachechemea kidogo kwa sababu wakati wanawaokoa aliruka dirishani akaumia mguu kidogo, lakini yuko salama,” alisema Balozi Bana.
Alipoulizwa endapo wamelipa fedha walizotaka watekaji hao, Balozi Bana hakuwa tayari kuzungumzia hilo, badala yake akasema Jimbo la Minna ndiyo wanaweza kulizungumzia, alisisitiza kwamba wametumia mbinu zote kuhakikisha wanaachiwa huru.
Kuhusu hatima ya Mtanzania huyo kurejea nchini, Balozi Bana amesema shirika lake la Wamisionari wa Afrika likiona inafaa limpe likizo ili arudi nyumbani akawatoe hofu wazazi wake na waumini waliokuwa wakimuombea.
Mahinini ni mzaliwa wa Kigoma katika Parokia ya Kabanga, pia ni mseminari, alipelekwa Nigeria na shirika hilo kwa ajili ya mwaka wa kichungaji kabla ya kuanza masomo ya Teolojia.
Wakati huohuo, shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers) lilitoa taarifa jana likishukuru kwa maombi yaliyowezesha kupatikana kwa vijana hao waliokuwa wametekwa nyara. Shirika hilo linaeleza kwamba wamepatikana wakiwa salama licha ya kupitia kipindi kigumu.
“Tukio hili lilipotokea, tuliwaomba msaada wenu na maombi. Kuachiwa kwao ni uthibitisho wa kujibiwa kwa maombi yetu. Hii ndiyo sababu tunarudi kwenu kutoa shukrani kwa kuwa nasi katika kipindi hiki kigumu cha giza na majaribu,” inaeleza taarifa hiyo na kuongeza:
“Tunawaombea kuongoka kwa wale wanaodhani njia rahisi ya kujipatia fedha ni kwa kuumiza wengine,” inaeleza taarifa hiyo.