Mtanzania kuanzia miaka 18 kuanza kulipa kodi

Wapambe wa Bunge wakimuongoza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kuingia bungeni kwa ajili ya kuwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali inakusudia kutoa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) kwa kila Mtanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kuanza kulipa kodi.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali inakusudia kutoa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) kwa kila Mtanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kuanza kulipa kodi.

Dk Mwigulu amebainisha hayo leo Jumanne Juni 14, 2022 bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/23.

Waziri huyo amesema ili kufikia azma hiyo wataanza kutoa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) kwa kila mtanzania  kuanzia umri wa kuanzia miaka 18 kwa utaratibu wa usajili wa namba ya utambulisho wa Taifa (NIDA) unaomtaka kila mwananchi mwenye umri huo wa au zaidi kujisajili.

“Napendekeza kuwa wale wote wenye NIDA kwa sasa (wanaofikia milioni 19 nchi nzima) wapatiwe namba ya TIN na itumike kwenye miamala yote inayofanyika katika ununuzi na mauzo yanayofanyika ndani ya nchi,”amesema

Waziri huyo amefafanua kuwa kila mwenye namba ya mlipakodi atapata makadirio yake kwa njia ya simu na kulipa kodi husika kwa njia ya mtandao.