Mtendaji wa kijiji afungwa miaka 20 jela kwa wizi

Muktasari:

  • Mtendaji huyo wa Kijiji cha Kainam wilayani Mbulu mkoani Manyara, Samwel Qambino amehukumiwa kwenda jela kwa kutiwa hatiani kwa makosa matatu hivyo kwa makosa hayo atatumikia miaka 20.

Mbulu. Mtendaji wa Kijiji cha Kainam wilayani Mbulu mkoani Manyara, Samwel Qambino amehukumiwa na mahakama ya wilaya hiyo kwenda jela kwa kifungo cha miaka 20.

 Qambino amehukumiwa kifungo hicho baada ya mahakama ya wilaya kumtia hatiani kwa makosa matatu yaliyokuwa yanamkabili ambapo kila kosa amehukumiwa kifungo tofauti.

Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Mbulu, Victus Kabigi ametoa hukumu hiyo jana Ijumaa Aprili 28, 2023 kwenye mahakama hiyo iliyopo mjini Mbulu.

Kabigi amesema katika shauri hilo mshtakiwa huyo alishtakiwa kwa makosa matatu ambayo ni ubadhirifu, matumizi mabaya ya madaraka na wizi katika utumishi wa umma.

Amesema katika shtaka la kwanza mahakama hiyo imemuhukumu kifungo cha miaka 20 jela, matumizi mabaya ya madaraka kifungo cha miaka 20 jela na wizi katika utumishi wa umma mwaka mmoja jela, hivyo atatumikia kwa pamoja miaka 20.

Hata hivyo, mahakama hiyo imemtaka mshtakiwa huyo kurejesha kiasi cha Sh3.6 milioni alizofanyia ubadhirifu au mali zake ziuzwe ili kufidia fedha hizo.

Awali, mwendesha mashtaka wa kesi hiyo Martin Makani ameieleza mahakama hiyo kuwa mshtakiwa huyo hana taarifa zozote za kufanya uhalifu hivyo hayo ni makosa yake ya kwanza.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo aliiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwani ni kosa lake la kwanza na pia familia yake inamtegemea.

Hakimu huyo amesema mahakama hiyo imetoa  adhabu hiyo kali baada ya mshtakiwa huyo kutiwa hatiani na pia ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wa serikali wanaofanya hivyo.