Mtoto aliyefanya mtihani wa la 7 gerezani ahukumiwa kifungo cha nje

Kunde Kilulu, anayekabiliwa na kesi ya mauaji alipozungumza na Mwananchi akiwa chini ya ulinzi katika Gereza Kuu Bariadi. Picha na Samirah Yusuph

Muktasari:

Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga imemhukumu mwanafunzi aliyefanya mtihani wa darasa la saba akiwa gerezani, Kunde Gambija Kilulu (15) kifungo cha nje miezi sita baada ya kumkuta na hatia ya kuua bila kukusudia.

Bariadi. Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga imemhukumu mwanafunzi aliyefanya mtihani wa darasa la saba akiwa gerezani, Kunde Gambija Kilulu (15) kifungo cha nje miezi sita baada ya kumkuta na hatia ya kuua bila kukusudia.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu Novemba 15, 2021 na Jaji Seif Mwishehe Kulita katika mahakama iliyoketi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu.

Jaji Kulita amesema ni mara ya kwanza kwa washitakiwa kutenda kosa na wamekiri kosa bila usumbufu wowote hivyo mahakama imeokoa muda pamoja na kuepuka ghalama za uendeshaji wa kesi.

Amesema mtuhumiwa namba moja Sayi Gisabu na namba mbili Kunde Kilulu walikutwa na hatia Novemba 8, 2021 ambapo kesi ya kuua bila kukusudiwa namba 66 ya mwaka 2021 iliposomwa kwenye mahakama kuu kwa mara ya kwanza.

Katika kesi hiyo watuhumiwa walikutwa na hatia ya kumuua bila kukusudia  Gegedi Kulabya (57) ambaye walimkuta faragha akiwa na binti wa familia ambaye ni dada wa mwanafunzi mwenye umri wa kitendo kilichomfanya baba kuchukua uamzi wa kushirikiana na watoto wake kumpiga mwanamme huyo na kumsababishia kifo.

Amesema mahakama imetoa adhabu kwa kuzingatia kuwa mshitakiwa wa pili ni mtoto anayetarajiwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza mwakani pia alishiriki mauaji kwa kufuata maelekezo ya mzazi ambaye aliongoza kwenda katika chumba cha dada yao.

Mshitakiwa wa kwanza ambaye ni baba mzazi wa Kunde Gambija Kilulu, Sayi Gisabu amehukumiwa miaka mitano jela na Kunde Gambija Kilulu atatumikia kifungo cha nje miezi sita kwa sharti la kutokutenda kosa lolote la jinai akiwa chini ya uangalizi wa maafisa wa ustawi wa jamii.

Kwa upande wake wakili wa upande wa utetezi Samwel Lugundija amesema hukumu imetolewa kwa kuzingatia kifungu cha 38 kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejeo mwaka 2019 na wamerizika na adhabu hiyo.

Kunde Gambija Kilulu ni mhitimu wa darasa la saba aliyefanya mtihani wa Taifa akiwa katika gazeti la Bariadi mkoani Simiyu akikabiliwa na kesi ya mauaji ambapo amefaulu kwa daraja B.